ILE hali ya kufanya kazi kwa mazoea (business as usual) iliyojengeka kwa baadhi ya watendaji wa Serikali leo imewatokea puani watendaji wa Manispaa ya Dodoma wakati Waziri Mkuu alipoamua kufanya ziara kukagua miradi ya maendeleo.
Akiwa katika eneo la kwanza ambalo alipangiwa kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Mkonze Jumamosi, Juni 7, 2014 Waziri Mkuu alipokea taarifa ya ujenzi wa kituo na kubaini kuwa hawajafanya chochote ili kutekeleza maagizo yake aliyoyatoa Machi 22, 2014.
Katika taarifa yake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe alimweleza Waziri Mkuu kwamba walifanya tathmini ya ujenzi wa kituo hicho na kubaini kuwa zinahitajika sh. Milioni 24.15 na kwamba maombi ya matumizi hayo yamepangwa kujadiliwa kwenye kikao cha kamati ya fedha na uongozi kitakachofanyika Juni 10, mwaka huu.
Akiwa katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji ambayo Kitaifa yalifanyika mkoani Dodoma, Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji jirani na kituo cha afya cha Mkonze na kubaini kuwa kuna hitilafu za ujenzi. Ndipo akaagiza kwamba ufanyike ukarabati na yeye akaahidi kuja kukagua ukarabati huo mwezi Juni, 2014.
Mara baada ya kusomewa taarifa ya mradi, Waziri Mkuu akahoji ni kwa nini hawajafanya chochote tangu alipotoa maelekezo Machi, mwaka huu. Hakupata jibu la kueleweka kutoka kwa viongozi wa wilaya na mkoa.
Waziri Mkuu aliwasalimia wananchi waliokuwepo kwenye eneo hilo na kuwaeleza kwamba hawezi kukagua kituo hicho ilhali hakuna kilichotekelezwa tangu afike hapo Machi mwaka huu.
Alisema haiwezekani yeye atoe maagizo katika kipindi chote hicho halafu kisifanyike kitu chochote. Akaondoka na kuendelea na ziara hadi kijiji cha Manzase ambako alikagua mradi wa kisima cha maji.
Mapema, katika taarifa yake, Mhandisi Kilembe alisema kituo hicho cha afya kilijengwa chini ya ufadhili wa ubalozi katika makubaliano yaliyofikiwa Novemba 11, 2009 kwamba ingetoa dola za marekani 84,307 sawa na sh. Milioni 152.86.
Hata hivyo, mara baada ya ujenzi kukamilika Agosti 29, 2012, kituo hicho kilipata nyufa nyingi hali iliyosababisha kifungwe na wananchi walitoa malalamiko yao kwa Waziri Mkuu Machi mwaka huu wakati alipokwenda kuzindua mradi wa maji kwenye kijiji cha Mkonze jirani na kituo hicho.
Akiwa katika kijiji cha Manzase Waziri Mkuu aliridhishwa na ujenzi wa mradi wa maji kwa ajili ya wakazi 9,000 wa eneo ambapo alielezwa kwamba utakamilika Julai 16, 2014.