Tajiri Afanya Ukatili wa Kutisha kwa ‘House Girl’ Atumia Pasi ya Moto…!

Yusta Lucas akionyesha makovu yake ya mgongoni ambayo aliyapata kwa kung'atwa na kuchomwa na pasi na mwajili wake.

Yusta Lucas akionyesha makovu yake ya mgongoni ambayo aliyapata kwa kung’atwa na kuchomwa na pasi na mwajili wake.


*Adaiwa kumng’ata, kumchoma pasi mtumishi wake kwa miaka mitatu

MFANYAKAZI wa ndani (house girl), Yusta Lucas (20) amekumbana na masahibu yanayofanana na yale ya mtoto Nasra Mvungi (4) aliyekuwa amefungiwa kwenye boksi kwa miaka karibu minne huko Morogoro. Huyu amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam akiuguza majeraha yanayotokana na kuteswa na kufungiwa ndani kwa miaka mitatu.

Binti huyo, mwenyeji wa Mkoa wa Tabora, katika Kijiji cha Kampala amedai kuwa amekuwa akiteswa na kufungiwa ndani ya nyumba na tajiri yake, Amina Maige wa Mwananyamala, Kwa Manjunju katika kipindi chote hicho. Amina anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa tuhuma hizo na amefunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014.

Akisimulia masahibu yaliyompata akiwa katika Wodi Namba Tatu ya hospitali hiyo, Yusta alisema: “Nililetwa Dar es Salaam mwaka 2010 kufanya kazi za nyumbani baada ya bosi wangu (Amina) ambaye ni binamu yangu kuzungumza na mama yangu na kuniomba nije kumsaidia kazi ndogondogo.”

Alisema aliishi vizuri na mwajiri wake huyo, lakini mwaka 2012 ndipo mambo yalipoanza kubadilika akidai kuwa Amina alianza kumwadhibu kwa kumng’ata na kumchoma kwa pasi kila alipomtuhumu kutokufanya kazi zake vizuri.

“Alikuwa akinichapa na kuning’ata sehemu mbalimbali wakati mwingine usoni, pia kunichoma kwa pasi yenye moto kila aliponituhumu kutokufagia au kupiga deki vizuri.”

Hakuwahi kupelekwa hospitali

Alisema licha ya kupata vidonda kutokana na adhabu hizo, mwajiri wake huyo hakuwahi kumpeleka hospitali na pale alipoona hali ni mbaya alimnunulia dawa… “Tunaishi wawili tu baada ya kuondoka mumewe na mtoto wake kumpeleka shule ya bweni… niliugulia hadi nikapona bila mtu mwingine kufahamu.”

“Akienda kazini anafunga geti na kunikataza kufungua hata kama mtu atagonga… sokoni nilikuwa naenda siku ambazo yeye yupo tu na huwa akiniamrisha niende haraka na kurudi pasipo kuzungumza na mtu yeyote.”

Alisema mwajiri wake huyo alikuwa akituma pesa za mshahara wake kwa mama yake akisema ndiye anayepaswa kulipwa, jambo ambalo anadhani limemfanya mama yake kuhisi mwanaye yuko katika mikono salama… “Kila alipotuma alipiga simu na kunipa niongee na mama kuhakikisha kama zimefika huku akinisimamia na baada ya hapo anachukua simu.”

Ataka kurudi kwao
Binti huyo ambaye sehemu kubwa ya mwili wake ina alama za kung’atwa meno na majeraha ya kuchomwa na pasi, alisema: “Ninaomba mtu yeyote mwenye hela, nataka nikitoka hapa hospitali nirudi Tabora kwa mama. Nina shaka na maisha yangu hapa kwa huyu mama… sitaki tena kubaki Dar es Salaam kutokana na mateso ninayoyapata.

Polisi wasema
Mkaguzi Msaidizi wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Kinondoni, Prisca Komba alisema taarifa za binti huyo ziliwafikia baada ya majirani kupeleka taarifa hizo katika Kikundi cha Kipange kilichopo Kwa Manjunju ambacho nacho kilitoa taarifa polisi na ndipo mtego wa kumnasa mwanamke huyo ukawekwa.

Majirani walichukua hatua hiyo kutokana na kusikia kelele za kilio mara kwa mara zikitokea ndani ya nyumba ya mtuhumiwa. “Tumekagua makovu na majeraha mbalimbali yaliyo katika mwili wake na kupata jumla kuwa yako 91,” alisema Komba na kuongeza:

“Toka jana amekuwa akinitaka nisiondoke mbali naye amekuwa na hofu, lakini sasa afadhali kidogo baada ya kumpatia ushauri na kumhakikishia kwamba hapa yuko salama.”

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Thobias Edoyeka alisema suala hilo linashughulikiwa na polisi pamoja na ustawi wa jamii, kauli iliyoungwa mkono na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mwananyamala, Rose Temu ambaye alisema wanafuatilia kwa karibu matibabu yake pamoja na usalama wake. “Hali yake ikishaimarika na kujiridhisha kuwa anaendelea vizuri, tutakuwa na jukumu la kumuunganisha na familia yake,” alisema.

Ofisa Muuguzi Msaidizi Wodi Namba Tatu ambayo ni ya kinamama, Rose Mussa alisema Yusta anaendelea vizuri.

“Anaendelea vizuri kwa kweli, jana (juzi) hakuwa hivi alikuwa mwoga hawezi kujieleza tofauti na leo (jana)… bado anaendelea na vipimo, tutakapoona anafaa kuruhusiwa tutafanya hivyo na kumkabidhi kwa ustawi wa jamii.”