Mahakama Yaondoa Kinga ya Wabunge Kushtakiwa

Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande

Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imefungua milango kwa mawaziri na wabunge kufunguliwa mashtaka kutokana na kauli watakazozitoa bungeni ambazo ni kinyume cha Katiba na Sheria. Mahakama Kuu ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa uamuzi wa pingamizi la awali katika kesi ya kikatiba iliyokuwa ikimkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lililowasilishwa na Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG, George Masaju.

Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 ilifunguliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliyeunganishwa kama mlalamikiwa wa pili.

LHRC na TLS walikuwa wakidai kuwa Pinda alivunja Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni, wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu. Hivyo, walikuwa wakiiomba mahakama, pamoja na mambo mengine, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru Pinda aifute hadharani.

Hata hivyo, Pinda na AG waliokuwa wakitetewa na DAG Masaju akisaidiana na Mawakili wa Serikali Wakuu (PSA, Gabriel Malata, Alecia Mbuya na Sarah Mwipopo), waliweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo, wakitoa hoja tano za kuomba kesi hiyo itupiliwe mbali.

Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kwamba kesi hiyo ni batili na iko mahakamani isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge, ya mwaka 1988.

Mawakili hao walidai kuwa Pinda analindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) na (2), ambazo zinamkinga mbunge kushtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, au alilolitenda, au alililoliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada au hoja.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake jana ilikubaliana na baadhi ya hoja za mawakili wa utetezi (Serikali) na kuitupilia mbali kesi hiyo, lakini ikatamka kuwa wabunge na mawaziri wanaweza kushtakiwa kwa kauli au jambo walilolitamka bungeni, linalokiuka sheria na haki za binadamu.

Uamuzi huo ulisomwa na Kiongozi wa Jopo la Majaji wa Mahakama Kuu, lililokuwa likisikiliza kesi hiyo, Jaji Kiongozi Fakih Jundu kwa niaba ya majaji wenzake, Agustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.

Katika uamuzi huo, majaji walikubaliana na hoja tatu za pingamizi kuwa walalamikaji katika kesi hiyo hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo na kwamba walikosea taratibu za ufunguaji wa kesi kama hizo kwa kuwa walikiuka amri na kanuni zinazoongoza Mashauri ya Madai (CPC).

Katika hoja ya kwanza kuwa Pinda kama mbunge analindwa na Katiba, jopo hilo lilisema kuwa ni kweli wabunge wanalindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) kuhusu haki na upendeleo (Previledge), yaani haki na uhuru wa mjadala na maoni. Hata hivyo, lilikataa hoja za utetezi kuwa wabunge wana kinga isiyo na mipaka ya kutokushtakiwa kwa kauli au jambo lolote walilolitamka bungeni.

Badala yake jopo hilo lilikubaliana na hoja za mawakili wa walalamikaji, kuwa japo wabunge wana kinga, lakini kinga yao ina mipaka na kwa kuwa inadhibitiwa na masharti ya ibara nyingine za Katiba na Sheria za Bunge. Walalamikaji walikuwa wakitetewa na Peter Kibatala, Fulgence Massawe, Harold Sungusia, Mpale Mpoki na Jeremiah Mtobesya.

Kuhusu hoja ya pingamizi kuwa walalamikaji hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo, mahakama ilikubali kuwa kwa walalamikaji katika kesi hiyo hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo. Ilifafanua kuwa anayepaswa kufungua kesi ni yule tu aliyeathirika na kauli iliyotolewa na mlalamikiwa na si mashirika, kwa kuwa kauli ya mlalamikiwa haikuyaathiri mashirika hayo yaliyofungua kesi.

Mahakama ilifafanua kuwa mtu aliyeathirika na kauli iliyotolewa bungeni anaweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge hasa kanuni ya 71 (1). Ilisema kwa kuwa kanuni hiyo haitoi nafasi kwa mashirika, basi mashirika yanaweza kufungua kesi mahakamani kwa kufuata taratibu za kisheria, ikiwa kauli iliyotolewa bungeni itakuwa imeyaathiri moja kwa moja.

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema kuwa ingawa kesi yao imetupiliwa mbali, lakini kitendo cha mahakama kutamka kuwa wabunge hawana kinga isiyo na mpaka na kwamba wanaweza kushtakiwa ni ushindi mkubwa.

Kwa upande wake Wakili Sungusia alisema kuwa wiki ijayo watakutana na jopo la mawakili ili kujadili uamuzi huo na hatua za kuchukua kama watakata rufaa Mahakama ya Rufani au la.

Katika pingamizi lao, mawakili wa utetezi pia walidai kuwa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani haijasainiwa kwa kuwa waliosaini si walalamikaji na kwamba hawajaonyesha kama wamepewa mamlaka ya kusaini kwa niaba ya walalamikaji.

Walidai kuwa walalamikaji ni taasisi yaani LHRC na TLS, lakini waliosaini ni Dk Hellen Kijo Bisimba kwa niaba ya LHRC na Wakili Francis Stolla (Rais wa TLS) kwa niaba ya TLS, lakini hawaonyeshi kama wamepewa mamlaka ya kusaini hati hiyo.

Pia mawakili wa walalamikaji walidai kuwa hati ya madai ina dosari za kisheria kwa kuwa kwa mujibu wa kanuni za Uendeshaji wa Mashauri ya Madai (CPC), hati inapaswa kueleza madai tu na si ushahidi, hoja wala maoni, walalamikaji wameelezea na maoni yao binafsi.

Upande wa walalamikaji katika majibu yao walidai kuwa walalamikaji wana haki ya kuwashtaki walalamikiwa. Wanadai kuwa kinga ya mbunge ina mpaka na inamlinda kwa shughuli za bunge tu na kwamba hati hiyo haina dosari huku wakidai kuwa hata kama zipo dosari za kisheria, basi zinaweza kurekebishwa.

Pinda alitoa kauli hiyo inayolalamikiwa, katika mkutano wa 11 wa Bunge wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni, Juni 20, 2013.

Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu kuhusu msimamo wa Serikali, pamoja na mambo mengine, malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara, kuwapiga wananchi.

“Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu… Eeh, hamna namna nyingine, eeh maana lazima tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.

“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi… wewe ndiyo jeuri zaidi… watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh… maana tumechoka,” inasomeka hati ya madai ikinukuu maneno ya Pinda.

CHANZO: Mwananchi