Zitto Atoa ya Moyoni, Kwenye Mazishi ya Mamayake…!

Mazishi ya Mama Zitto Kabwe, Shida Salum, aliyefariki juzi jijini Dar es Salaam.

Mazishi ya Mama Zitto Kabwe, Shida Salum, aliyefariki juzi jijini Dar es Salaam.

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amewaomba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba watakaporejea Agosti 5, wapitishe rasimu ya pili ya katiba kama njia ya kumuenzi mama yake Shida Salum, aliyefariki juzi jijini Dar es Salaam.

Shida, aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuwa mjumbe wa Bunge hilo kutoka kundi la wajumbe 201 ambapo aliwawakilisha walemavu, japo alishindwa kuhudhuria kikamilifu kwenye vikao kutokana na saratani ya shingo ya kizazi iliyokuwa ikimsumbua.

Licha ya kuhudhuria vikao vya mwanzo vya kutunga kanuni, hakupata fursa ya kuapishwa baada ya kuzidiwa akiwa mkoani Dodoma ambako walimpeleka kwenye hospitali ya mkoa huo kabla ya kumhamishia jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Kauli ya Zitto
Akizungumza katika mazishi ya mama yake jana mkoani Kigoma, Zitto alisema Watanzania wengi hivi sasa wanataka kupata katiba mpya yenye kujali masilahi yao, hivyo ni vema wajumbe wa Bunge Maalumu wakalitimiza jukumu hilo ambapo pia itakuwa ni sawa na kumuenzi mama yake.

Zitto alisema kuwa nyendo za mama yake ndizo zilimfanya awe mwanasiasa imara na kufikia hatua hiyo na kuongeza kuwa ni pigo kubwa kwa familia yao kwani alikuwa mshauri. Mwakilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekiel Wenje, alisema kuwa msiba huo ni mzito na wameondokewa na mtu muhimu katika chama. Wenje alisema kuwa kifo cha Shida ni pigo kwa CHADEMA na kufananisha na mshumaa uliokuwa tegemeo ambao umezimika katikati ya giza totoro.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Naibu Spika, Job Ndugai, aliyesema kuwa kifo cha mjumbe huyo wa Bunge Maalumu la Katiba ni pigo kwa kuwa alikuwa mwanahoja aliyefanya Bunge hilo kuchangamka.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, aliyewakilisha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema Shida ameondoka katika kipindi ambacho watu wengi walitarajia angekuwa msaada mkubwa zaidi kwa taifa.

“Kwa macho ya kibinadamu tulidhani Shida angekuwa msimamizi hodari wa walemavu aliokuwa akiwawakilisha, lakini Mungu amepanga, hivyo ni fumbo kwetu,” alisema.

Miongoni mwa watu waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya, Mbarouk Suleiman, kwa niaba ya kambi ya upinzani bungeni, Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, Makame Mbarawa, aliyewakilisha wabunge wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa chama cha ACT, Samson Mwigamba na Vita Kawawa, aliyewakilisha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wabunge wengine waliohudhuria mazishi hayo ni David Kafulila, Moses Machali wa NCCR-Mageuzi, Ismail Aden Rage, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Kigoma Malima na Deo Filikunjombe.

Shida Salum, alizaliwa Julai 7, 1950 mkoani Kigoma na kupata elimu ya sekondari Tabora. Enzi ya uhai wake alishawahi kuwa mtumishi wa Shirika la Forodha mwaka 1970 na mwaka 1975 alikuwa mwakilishi wa Taasisi ya Action Aids. Hadi mauti yanamkuta alikuwa Mjumbe wa Baraza la CHADEMA na Mwenyekiti Wa Chama Cha Walemavu (Chawata) na ameacha watoto 10.

CHANZO; Tanzania Daima