WATU wanaokunywa dawa za kufubaza makali ya Virusi Vya Ukimwi(ARV) huku wakitumia pombe kwa wingi wametajwa kujiweka katika hatari zaidi. Wanaweza kuharibu dozi na kusababisha kushuka kwa kinga ya mwili, kuongeza kiwango cha sumu mwilini, kuharibu ini na figo. Watalaamu wa afya wanasema kuwa kiasi kidogo cha pombe kwa mtu anayeishi na VVU, hakina madhara jambo ambalo pengine limesababisha watumiaji wengi wa ARV kubobea katika ulevi na kuhatarisha afya zao.
Mtafiti wa Masuala ya Ukimwi, Kutoka Taasisi ya Utafiti wa Tiba nchini, NIMR, Dk Edward Maswanya anasema hairuhusiwi hata kidogo kuchanganya pombe na dawa, kwani pombe huua nguvu ya dawa. Anasema pombe inasababisha usugu wa dawa hali ambayo huchangia dawa hizo zisifanye kazi yake inavyotakiwa.
“Sioni umuhimu wa mtu anayetumia ARV kunywa pombe, anajiua mwenyewe kwa sababu anasababisha usugu wa dawa na anaweza kupata mabadiliko makubwa kwenye mwili yatakayomuathiri,” anasema.
Utafiti mwingine uliochapishwa na Jarida la Tiba la Boston, 2013 uligundua kuwa karibu nusu watu wanaoishi na VVU na ambao wanatumia ARV, huacha kutumia dawa baada ya kulewa sana na kuharibu ratiba ya dozi zao. Kwa kufanya hivyo utafiti huo uligundua kuwa wanaharibu kiwango chao cha kinga(CD4). Katika utafiti huo, watafiti walitumia sampuli ya watu 178 wanaokunywa pombe na kutumia ARV, na kuwafuatilia kwa miezi 12. Walibaini kuwa mtu mmoja kati ya wanne, aliacha kutumia dawa jambo lililochangia kushuka kwa kinga ya mwili.
“Asilimia 51 ya watumiaji wa pombe wanaotumia ARV, walichangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kinga ya mwili hadi CD4 chini ya 200,” unasema utafiti huo.
Mfamasia katika Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa (CDC) cha jijini Dar es Salaam, Charles Lymo anasema watumiaji wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi, wana kipimo maalum cha kunywa pombe ambacho hakitakiwi kuzidi lita 1.6. Anasema ingawa hakuna athari za moja kwa moja za kuchanganya ARV na pombe, lakini unywaji wa pombe kwa wingi unaingiliana na utendaji kazi wa dawa hizo.
“Watu wanaotumia ARV na wakinywa pombe ni wengi, wapo wanaofanya kwa siri na wengine sisi watoa huduma tunawafahamu kuwa ni walevi kupita kiasi na tunawashauri kupunguza,” anasema.
Anasema madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kwa kutumia ARV na pombe ni kuwa mtu anayekunywa pombe hukojoa mara kwa mara, hivyo endapo amekunywa ARV basi haziwezi kufanya kazi kwa sababu hutolewa nje kwa njia ya mkojo. Dk Isaack Maro anasema, mtu anayekunywa ARV, aghalabu husahau kunywa dawa pindi anapolewa jambo linalosababisha utendaji kazi mbovu wa dawa.
“Ukilewa unaweza usimeze dawa, usipomeza dawa unatengeneza usugu na pengine dawa zisifanye kazi kabisaa,” anasema Dk Maro.
Kamishna wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI TACAIDS, Dk Violet Bakari ametahadharisha uwezekano wa kutokea vifo zaidi na kutetereka kwa afya za watumiaji wa ARV ikiwa hawatapunguza matumizi ya pombe. Anasema ingawa kwa maeneo ya baridi baadhi ya watumiaji wa ARV wamekuwa wakisingizia hali ya baridi kuchangia unywaji wa pombe, amesema vivyo hivyo kwa maeneo ya joto pia imebainika watumiaji wa ARV wamekuwa watumiaji wa kileo hali ambayo amesema isitumike kama kisingizio cha kuhalalisha kuathiri afya zao.
Dk Bakari anasema uzoefu unaonyesha kadiri wanavyotumia dawa hizo na kuona afya zao zikiimarika, ndivyo wengi wao walivyojiingiza kwenye matumizi ya pombe hali ambayo amesema hawajatambua madhara yake kiafya na akawasihi afya zao zinazoimarika ziendane na uzalishaji kwa ajili kujiweka vyema kiuchumi.
“Lengo la kuwawezesha kupata dawa hizo ni kuimarisha kinga zao na kuwawezesha kutumia fursa ya afya bora katika kuendelea kutoa mchango wao kwa taifa na familia zao, tofauti na mtazamo wa wengi wao kuelekeza nguvu zao katika matumizi makubwa ya pombe,” anasema.
Mpango wa Kudhibiti Ukimwi nchini (NACP) wanaeleza kuwa pombe inasababisha madhara kwenye ini na kwamba baadhi ya dawa za Ukimwi ili zifanye kazi kikamilifu ni lazima zipitie kwenye ini na kwa mlevi linaweza kuwa na matatizo. Kwa mujibu wa NACP, matumizi ya ARV, kwenda sambamba na unywaji wa pombe husababisha usugu na kuzalisha virusi hatari zaidi. Vituo kadhaa vya kutolea huduma za afya, kama ugawaji wa dawa za ARV, vilikiri kuwa watumiaji wengi wa ARV wanakunywa pombe.
“Wengi wanakunywa pombe baada ya kuona kuwa wamepata nafuu kutokana na ARV, lakini wakinywa zaidi pombe wanashindwa hata kufuata ratiba ya dawa na kusababisha virusi vijipange zaidi na kuwa sugu,” alisema Dk Akbar Nurul wa Hospitali ya Buguruni.
Lakini wataalamu wa afya wanadai kuwa madhara ya moja kwa moja ya ARV na pombe hutokana na uzembe au kusahau kunywa dawa. Kwa mfano, mtu akilewa kupita kiasi usiku wa jana, anaweza akasahau kunywa dawa kama dozi yake inavyomuelekeza, jambo linalosababisha kujenga usugu wa dawa na kuongezeka kwa idadi ya virusi mwilini.
ARV na pombe huleta imani?
Zibarikiwe dawa za kufubaza makali ya Ukimwi(ARV) ambazo zimesaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi, hata hivyo ARV huenda kikawa chanzo cha kuenea kwa maambukizi zaidi baada ya kuibuka kwa imani kuwa mtu anayetumia ARV hawezi kunywa pombe.
Imani hiyo imesababisha watu kuamini kuwa mtu akinywa pombe basi hana VVU na hilo limechangia wanafunzi, vijana kwa wazee kujikuta wakijihusisha kimapenzi bila kutumia kinga na watu wanaoishi na VVU.
CHANZO: Mwananchi