Wabunge Upinzani Watoka Bungeni, Zitto Awaita Wanaroho Mbaya, Pinda Atoa Kauli ya Serikali

Moja ya picha ikionesha baadhi ya wabunge wa upinzani wakitoka bungeni, siku za nyuma.

Moja ya picha ikionesha baadhi ya wabunge wa upinzani wakitoka bungeni, siku za nyuma.


Na Mwandishi Wetu

WABUNGE wa Kambi ya Upinzani Bungeni wametoka nje ya Bunge la Bajeti leo jioni mjini Dodoma ikiwa ni ishara ya kususia Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa madai hoja zao wanazowasilishwa zinapuuzwa. Wabunge hao wengi wakiwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi, CUF na NCCR-Mageuzi isipokuwa John Cheyo wa UDP na Augustine Mrema wa TLP wamesusia bajeti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo aliyoiwasilisha tangu jana.

Madai makubwa ya wabunge hao kabla ya kutoka bungeni ni kwamba hawapo tayari kushiriki kupitisha bajeti hiyo ambayo wanadai ndani ya taasisi hiyo kuna vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na baadhi ya viongozi likiwemo suala la IPTL, ilhali hoja zao zikipuuzwa.

Hata hivyo kabla ya kutoka mapema majira ya asubuhi msemaji wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika (MB) aliwasilisha bajeti mbadala na baadhi ya wabunge wa upinzani kuanza kuchangia bajeti kabla ya jioni kujitoa na kususia hata kusikiliza majibu ya hoja zao toka kwa Waziri Prof. Muhongo.

Akizungumza Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe kujibu hoja zilizotolewa na upinzani zikimtuhumu kuhusika kutumia vibaya nafasi yake na kujipatia fedha kupitia kampuni ya LekaDutigite alisema tuhuma zilizotolewa ni siasa za maji taka na hazina ukweli wowote zaidi ya chuki na roho mbaya.

“…Nasikitika kwamba katika hali niliyonayo ya kumuuguza mama yangu naingizwa kwenye siasa za majitaka. Kampuni ya Leka Dutigite inamilikiwa na wasanii. Gombe Advisors ni kampuni isiyofanya faida (Company limited by guarantee) na haina maslahi yeyote ya kibiashara.”
“Wasanii wa Kigoma wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo zinajulikana na zipo. Leo mpigie simu mfanyakazi yeyote wa NSSF utasikia kazi ya wasanii hao. Kwa namna yeyote ile hii ni ishara ya kukosa ubinaadamu maana waliyoyasema wanajua sina faida yeyote ya kifedha Leo wala kesho kwa Leka Dutigite na Gombe Advisors.”

“Kipindi ambacho mama yangu yupo mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya chama chao, pole ninayopewa ndio hiyo. Hakuna namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi. Hata hivyo, ni vema CAG afanye ukaguzi haraka sana na mimi binafsi nitawajibika iwapo itaonekana kwa namna yeyote ile nina maslahi ya kifedha katika Leka Dutigite na gombe advisors..Ni ushetani. Ni roho mbaya. There are limits to political attacks,” alisema Zitto ambaye kwa sasa anamgogoro na chama chake.

Akitoa kauli ya Serikali mara baada ya bunge kupitiza bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alionesha kitendo cha kukerwa na wabunge waliotoka nje ya bunge na kudai hali hiyo imekuwa kama mchezo kwani kila wanapowasilisha hoja na ikashindwa hukimbilia kutoka nje ya bunge.

Alisema inasikitisha sana kuona upinzani wamewasilisha hoja zao zote na kuchangia lakini ghafla wameamua kutoka nje ya bunge “…inawezekana kweli kanuni zinaturuhusu lakini haiwezekani kila unapowasilisha hoja na ukiona inashindwa njia rahisi iwe kutoka nje ya bunge…nimeona niliseme hili ili Watanzania waone si jambo zuri kwa viongozi kama hao kutoka, tunabishana hapa kwa hoja, sasa kama umeleta hoja unajenga hoja haina sababu ya kutoka…,” alisema Pinda.

Alishauri ipo haja ya kuziangalia kanuni za bunge kama zinaonekana kutumika ndivyo sivyo ili zirekebishwe. Aliongeza kuwa Wizara ya Nishati na Madini ina kila sababu ya kupongezwa kwa mambo ambayo wamefanya hadi sasa na hata kama baadaye wataonekana wamekosea wataadhibiwa kwa mujibu wa taratibu.