Upinzani Waibua Ufisadi Wizara ya Uchukuzi

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba.

KAMBI rasmi ya upinzani bungeni imeibua ufisadi wa kutisha, kwamba Wizara ya Uchukuzi iliiagiza Mamlaka ya Bandari (TPA), ilipe gharama za sh milioni 11.164 katika Hoteli ya New Africa kwa ajili ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba.

Ufisadi huo uliibuliwa jana bungeni na Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye hotuba yao kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2014/15. Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema malipo hayo kwa ajili ya malazi, yalifanyika Machi 28 mwaka jana.

“Mheshimiwa Spika, Machi 14 2013, Wizara ya Uchukuzi iliandika barua yenye kumb. Na. CB 230/364/01/A iliyoomba PTA ilipe gharama ya sh milioni 11.164 katika Hoteli ya New Africa kwa ajili ya Naibu Waziri wa Uchukuzi. Malipo haya yalilipwa na Bandari Machi 28, 2013. Malipo hayo hadi leo hayana maelezo.

Machali alisema ufisadi huo umeainishwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kwa mwaka huu wa fedha. Alisema katika taarifa ya CAG, haijaelezwa fedha hizo zililipwa kwa ajili ya shughuli gani zilizokuwa zikitekelezwa na Naibu Waziri huyo na shughuli hizo zilikuwa na maslahi gani kwa umma.

Kwa mujibu wa Machali, taarifa ya CAG ya mwaka 2012/2013 imebainisha kwamba kuna matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Wizara ya Uchukuzi. Alisema wizara hiyo imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali kwa TPA ikiiagiza kufanya matumizi kwa ajili ya wizara hiyo kinyume na taratibu za utawala bora.

Katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka 2013, Machali alisema CAG alibaini kuwa sh milioni 44.320 zililipwa na Bandari kwa niaba ya wizara hiyo. Alisema kuwa Bandari ililipa sh milioni 18.156 kwa ajili ya kugharimia safari ya Naibu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Uchukuzi ya kwenda nchini Ghana kwa safari ya kikazi.

Alisema TPA ilipata mwaliko wa watu wanne kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Afrika yaliyofanyika huko Accra, Ghana kuanzia Juni 16 hadi 23, 2013. Aliongeza kuwa TPA ilimteua Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu kuiwakilisha Bandari na wizara ikamteua Naibu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu ili kuiwakilisha wizara katika maadhimisho hayo ambapo gharama za washiriki wote wawili ziligharamiwa na Bandari.

Alisema taarifa ya CAG inaendelea kubainisha kwamba jumla ya sh milioni 15 zililipwa kwa Wizara ya Uchukuzi Machi 25 mwaka 2013 kwa ajili ya Baraza la Wafanyakazi lililofanyika Aprili 25, 2013.

CHANZO; Tanzania Daima