Chuo cha Mwalimu Nyerere kufungua tawi Zanzibar


Mkuu wa Chuo hicho, Dk. John Magotti

Benjamin Sawe, Maelezo

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinatarajiwa kufungua rasmi tawi lake la Zanzibar ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo hicho. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo hicho Dkt.John Magotti katika sherehe ya ufunguzi wa Maadhimisho ya miaka 50.

Dkt Magotti alisema tawi hilo la Zanzibar litafunguliwa rasmi katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 ambapo litaanza kutumika katika mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Alisema katika kuadhimisha miaka 50 ya chuo hicho idadi ya udahili wa wanafunzi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika kipindi cha mwaka wa masomo 2005/2007 chuo kilikuwa na wanafunzi 402 ikilinganishwa na wanafunzi 2087 katika mwaka wa masomo 2010/2011.

Aidha idadi ya wafanyakazi imeongezeka kutoka wafanyakazi 53 katika mwaka 2005/2006 hadi kufikia wafanyakazi 147 mwaka huu.

“Kwa kweli katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo chetu na miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika chuo chetu kimepata mafanikio makubwa sana”.Alisema Mkuu wa Chuo.

Alisema wakati wa maadhimishi ya miaka 50 ya chuo hicho wamekabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili ya muasisi wa chuo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.

Alizitaja changamoto nyingine ni pamoja na kuandaa viongozi wa taifa hasa katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi vya siasa na kusema maandalizi ya viongozi ni muhimu katika kulinda maslahi ya taifa.

Katika sherehe hizo Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba alisema viongozi wa sasa wamekuwa hawazingatii maadili na nidhamu katika utendaji kazi na wamekuwa wabinafsi.

Akitolea mfano wa shughuli za Bunge zinazoendelea Jijini Dodoma Warioba alisema Bunge siku zote limekuwa ni kioo cha jamii kwani jamii nzima imekuwa ikijifunza kutoka kwa viongozi hao wan chi.

Alisema imekuwa ni aibu kubwa kwa baadhi ya wabunge kurushiana maneno bila kufuata kibali na kanuni za bunge wakati wa shughuli za bunge na wamekuwa wakijiaibisha wenyewe pamoja na muhimili huo.

Aidha Warioba alisema katika kipindi cha Mwalimu Nyerere, viongozi wa nchi walikuwa na nidhamu ya hali ya juu kwani walikuwa ni wazalendo na wanamshikamano kwa taifa.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho wameiomba serikali kuwarudisha viongozi waliokosa maadili chuoni hapo ili waweze kufundishwa maadili upya kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Chuo cha kilianzishwa tarehe 29, Julai 1961 kwa ushirikiano wa wananchi na makampuni binafsi.