BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo limetoa utaratibu mpya wa kuwabana watendaji wa vijiji na kata wasio toa taarifa za mapato na matumizi kwa wanakijiji wao ambapo kwa sasa watakuwa wakiwasilisha taarifa hizo katika kikao cha awali cha baraza la madiwani.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango, Protasi Lyakurwa ambaye pia ni diwani wa Kata ya Ngoyoni wakati alipokuwa akiwasilisha maazimio ya kamati hiyo katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani.
Lyakurwa alisema kuwa utaratibu huo mpya utaanza kutumika kuanzia mwezi Julai ambapo maofisa watendaji wa kata ndio watakaokuwa wakiwasilsha taarifa za mapato na matumizi katika kata zao kwenye kikao cha awali cha baraza la madiwani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Anthoni Tesha alisema kuwa wapo baadhi ya watendaji wa vijiji na kata ambao hawaitishi mikutano kwa wakati na kuijsahau kuwa wao ni watendaji wa halmashauri na utaratibu huo mpya utasaidia kuwabana.
Aidha katika hatua nyingine Tesha amemtaka mhandisi wa Maji wa wilaya ya Rombo, Andrew Tesha kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati uliopangwa ili kuondoa adha ya maji inayowakabili wananchi wa wilaya hiyo hususani katika maeneo ya vijiji vya ukanda wa chini.
Wakati huo huo, wajasiriamali wadogo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wameshauriwa kutokata tamaa na badala yake wawe wepesi wa kujaribu kufanya mambo bila woga. Ushauri huo umetolewa na mwezeshaji wa Mafunzo ya ujsiriamali kutoka shirika linalohusika na afya ya akina mama na watoto wadogo la FLEMAFA, Nicolina Mtatifikolo wakati alipokuwa akizungumza katika semina ya Mafunzo ya ujasiriamali kwa wanachama wa mtandao wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na asasi zinazoshughulika na mwitikio Dhidi ya Virusi vya ukimwi na UKIMWI ambayo imefanyika katika ukumbi wa kituo cha waalimu wilayani Rombo.
Aidha Mtatifikolo amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia ubora wa bidhaa watakazozitengeneza ili waweze kupata masoko ndani na nje ya wilaya ya Rombo. Pia ametoa ushauri kwa kwa wajasiriamali kuwa wepesi wa kutafuta masoko wenyewe badala ya kutegemea kutafutiwa masoko.
Awali akifungua mafunzo hayo ya Siku tatu Kaimu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo, Protas Lyakurwa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti ukimwi wilayani Rombo amewataka wajumbe wa mafunzo hayo watumie elimu watakayoipata kwa kuwafundisha watu wengine ili elimu hiyo iwe endelevu.