Ikulu Yatoa Pole Kifo cha Mwandishi wa Habari

Maximilian John

Maximilian John


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari Dk. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mpiga picha wa kituo cha television cha Mlimani, Ndugu Maximilian John kilichotokea alfajiri ya kuamkia leo tarehe 24 Mei,2014..
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Bwana Maximilian kilichotokana na maradhi ya Moyo, Sukari na Shinikizo la damu. Kifo hicho ni pigo na pengo kubwa kwa tasnia ya habari hapa nchini,”Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo.
“Bw. Maximilian atakumbukwa kwa uchapakazi wake na uhodori katika kazi zake siku zote. Kifo ni maandiko ya Mwenyezi Mungu hivyo hatuna budi kumshukuru kwa yote.
“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia ya Ndugu Maximilian, pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mzazi na mhimili wa familia. Aidha, salamu hizi ziwafikie pia wanahabari wote, wafanyakazi wenzake, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
Nakuomba uwajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu. Ninaungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.
Ndugu Maximilian John ameacha mke na watoto wanne.