BRN Sio Kauli Mbiu ya Kisiasa

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete


 
Na Mwandishi Wetu
 
MPANGO wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulioanzishwa na Serikali ya Tanzania sio kaulimbiu ya kisiasa kwa kuwa umedhamiria kusaidia kuyabadili maisha ya Watanzania moja kwa moja.
 
Hayo yalisemwa Dar es Salaam leo jijini Dar es Salaam na watendaji wandamizi kutoka Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekelezaji wa Miradi (PDB), walipokuwa wakihojiwa katika kipindi cha Makutano Show kinachorushwa na Radio Magic FM.
 
PDB ni kitengo kipya kilichoanzishwa chini ya Rais kusimamia Mpango wa BRN ili kuchagiza ufanisi wa kasi na viwango katika sekta sita zilizochaguliwa na elimu, maji, kilimo, Nishati, usafirishaji na ukusanyaji wa fedha.
Akizungumzia kuhusu Mpango huo, Bw. Mugisha Kamugisha alisema BRN imeweka malengo magumu kuyafikia kwa sababu wananchi wanahitaji maendeleo.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukusanyaji Mapato wa PDB, Bw. Lawrence Mafuru alisema katika eneo la ukusanyaji mapato, BRN inalenga kusaidia kupunguza nakisi katika Bajeti ya nchi kwa kuibua mikakati mipya ya mapato.
 
“Katika eneo la ukusanyaji wa fedha, BRN, imekuja na mtazamo mpya na mikakati mipya. Tunaamini kuwa zipo njia mpya za kikodi na zisizo za kikodi ambazo zinaweza kuliongezea Taifa mapato na tumejiwekea lengo hilo la trilioni 3,” Bw. Mafuru alisema.
 
Aliongeza kuwa ili kuongezeka kwa mapato ya Serikali Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itafanyakazi kwa karibu na PDB kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa.
 
Aliutaja mkakati mwingine wa kufikia hilo ni kuhakikisha makampuni ya umma ambayo yanazalisha faida yanalipa gawio kwa Serikali na pia kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi.