RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Meja Jenerali, Saidi Saidi Kalembo kuomboleza vifo vya watu 10 vilivyotokana na ajali mbaya ya barabarani iliyotokea usiku wa tarehe 28 Julai, 2011 katika Barabara ya Moshi – Arusha maeneo ya Kibosho Road mkoani humo.
Ajali hiyo ilihusisha magari manne. Katika ajali hiyo, gari aina ya Mitsubishi Fuso la Kampuni ya LIM Safari lililokuwa katika mwendo kasi likiwa limebeba wafanyakazi wa shamba la Kahawa la Kilimanjaro Plantation Limited, lilipoteza mwelekeo na kuligonga gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado.
Baada ya kuigonga Prado, gari hilo lilirudi tena barabarani na kuparuzana na basi la Scania la Kampuni ya Fresh Coach na baada ya kulipita basi hilo, ndipo Fuso hiyo ilipogongana ana kwa ana na lori jingine aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa limebeba shehena ya nyanya. Lori hilo lilipinduka na kuliangukia basi na kusababisha vifo vya watu 10 papo hapo, akiwamo dereva wa gari lililosababisha ajali ambaye amefia hospitali. Watu wengine 24 kujeruhiwa katika ajali hiyo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za vifo vya watu 10 vilivyosababishwa na ajali mbaya ya barabarani”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake hizo na kuongeza, “kwa mara nyingine ajali hii imeleta simanzi na huzuni kubwa isiyokuwa ya lazima kabisa kwa familia za wafiwa ambao ghafla wamejikuta wakipoteza ndugu zao.”
Rais Kikwete amemuomba Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa wa Kilimanjaro kumfikishia salamu zake za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wote waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hiyo.
Aidha amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi chote cha maombolezo huku akiwahakikishia kwamba yeye binafsi yuko pamoja nao katika msiba huo mkubwa. Kwa upande wa watu 24 waliojeruhiwa, Rais Kikwete anawaombea kwa Mola wapone haraka, ili waungane tena na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao na hivyo kuweza kuendelea na shughuli zao za kawaida za maisha yao.
Rais Kikwete amesema ni jambo la kusikitisha sana kuwa katika siku za hivi karibuni Taifa limeshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ajali za barabarani, ambapo nyingi ya ajali hizo kama hii iliyotokea mkoani Kilimanjaro, zinasababishwa na uzembe wa madereva.
Amezitaka mamlaka zote zinazohusika na utekelezaji wa Sheria ya Usalama Barabarani kutathmini upya utendaji wao wa kazi kwa lengo la kuongeza jitihada za kuisimamia kikamilifu Sheria hiyo, na kuimarisha mbinu za kukabiliana na ajali zinazotokea, ili wananchi wawe na uhakika na usalama wa maisha yao na mali zao wakati wote wanaposafiri.
Rais Kikwete amemaliza rambirambi zake kwa kusisitiza: “Naelewa fika machungu ya watu wote waliopoteza wapendwa wao katika ajali hii. Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke mahali pema peponi roho za marehemu wote. Amina.”