Frank Mvungi – Maelezo
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mgeni rasmi katika zinduzi wa Chapisho la Tatu la Taaurifa za msingi za Kidemografia, kijamii na kiuchumi linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 katika ngazi ya Taifa.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Hajjat Amina Mrisho Said wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ambapo uzinduzi huo utafanyika Mei 25, mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere uliopo Dar es salaam.
Hajjat Amina alisema kwa kifupi chapisho hilo, linatoa viashiria mbalimbali ambavyo ni pamoja na ongezeko la idadi ya watu,mgawanyo wa watu kwa umri na jinsi,muundo wa kaya,hali ya ndoa,hali ya ulemavu,idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi na wale wenye vyeti vya kuzaliwa na wasionavyo.
Alivitaja viashiria vingine ni vizazi na vifo,uhai wa wazazi,kujua kusoma na kuandika,shughuli zaki uchumi,hali ya makazi,mifuko ya hifadhi ya jamii na umiliki wa vifaa na huduma katika makazi.
Akifafanua zaidi kuhusu siku hiyo Hajjat Amina amesema watu wapatao 500 wanatarajiwa kushiriki katika uzinduzi huo wakiwemo viongozi wa ngazi za juu Serikalini, Mabalozi na Wadau wa maendeleo.
Hajjat Amina aliongeza kuwaViongozi wengine watakaoshiriki ni wa Dini, vyama vya Siasa na Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Pamoja na wadau wa Takwimu nchini.
Chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, kijamii na kiuchumi linalotokana na Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 ni mwendelezo wa machapisho mbalimbali yanayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama ilivyoainishwa kwenye kalenda ya machapisho ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.