UDA Kutumiwa na Wanafunzi kwa Vitambulisho Maalum

Mabasi ya UDA.

Mabasi ya UDA.

Na Anna Nkinda – Maelezo

WILAYA ya Kinondoni kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaandaa mkakati wa kusafirisha wanafunzi kwa vitambulisho maalum vya wanafunzi kwa bei naafuu kwa kutumia mabasi ya UDA  kwenda shule za pembezoni. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Ofisa Elimu Sekondari wilaya ya Kinondoni Omath Sanga wakati akisoma taarifa ya Idara ya Elimu kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipoitembelea shule ya Sekondari ya Kata ya Salma Kikwete iliyopo Kijitonyama wilayani humo.

Sanga alisema wanafunzi hao ambao wanatumia usafiri wa mabasi zaidi ya moja kwenda shule kwa siku kutoka majumbani kwao kuelekea maeneo ya Goba, Fahari, Kinzudi, Mabwe, Kisauke, Njechele, Mabibo, Malambamawili, Hondogo, Gogoni, Kibwegere na Kibweheri mara baada ya kukamilika kwa vitambulisho bivyo watalipa nauli ya shilingi 200 kwenda na 200 kurudi.

“Mwanafunzi atatumia kitambulisho maalum ambacho kitamuwezesha kupanda zaidi ya basi moja la UDA kutoka nyumbani hadi kufika shuleni kwa gharama ya shilingi 400 kwa siku hii ni kwenda na kurudi tofauti na ilivyo sasa wanatumia  fedha nyingi katika nauli kwani tatizo la usafiri kwa wanafunzi limekuwa ni moja ya changamoto inayoikabili wilaya yetu”, alisema Sanga.

Aidha alisema changamoto zinazoikabili idara hiyo ni upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari, vyumba vya madarasa, madawati na maabara kwa baadhi ya shule za msingi na Sekondari na ukosefu wa usafiri kwa wanafunzi wanaosoma shule za pembezoni.

Alisema mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ni wilaya hiyo imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na kukabiliana na uharibifu wa miungombinu. Vilevile wanashirikiana na wanajamii kwa ajili ya kuchangia ununuzi wa madawati.

Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)  aliwataka wanafunzi hao kuitumia Sayansi na Teknolojia kutafuta elimu na siyo tofauti kwani Dunia ya leo inahitaji mtu mmoja kuwa na utaalam wa namna nyingi ili aweze kufanikiwa na kuwa kivutio katika soko la ajira na kujiajiri.

Vilevile kuweza kwenda na wakati kulingana na mabadiliko jambo la muhimu ni kutokata tamaa mapema  na kutojiweka nyuma kwenye elimu yoyote yenye faida maishani.

Mama Kikwete alisema lengo kuu la elimu ni kuhakikisha  mwanadamu anapata maendeleo endelevu katika maisha yake ya uzima wa sasa na wa abaadaye, ili kuweza kulinda na kudumisha utu wake pamoja na kuendelea kuimarisha hazi zake za msingi kwani maisha ya mtu aliyesoma ni tofauti na maisha ya mtu asiyesoma.

“Kila mtu anapaswa kuhakikisha kuwa elimu anayoipata inamsaidia kuchangia maendeleo ya jamii husika, sanjari na kukua uelewano, uvumilivu na urafiki kati ya watu wa mataifa mbalimbali na kwa njia yah ii wau wanaweza kujenga misingi ya haki na amani,” alisema Mama Kikwete.

Akiongea kwa njia ya simu Mwenyekiti Mtendaji wa UDA Robert Kisena alisema vitambulisho hivyo ni maalum kwa ajili ya wanafunzi kutoka wilaya zote za Mkoa wa Dar es salaam ambazo ni Ilala, Temeke na Kinondoni wanasoma shule za Sekondari zilizopo pembezoni mwa mji.

“Wanafunzi watakaotumia vitambulisho hivi ni wale wanaotoka umbali wa km 30 hadi km 60 kutoka nyumbani hadi shuleni ingawa katika makubaliano ya awali ilikuwa ni walipe nauli ya shilingi 200 na kwa wanafunzi wasio na uwezo wasilipe nauli lakini kampuni yangu itaangalia kama ikiwezekana  wasilipe nauli kabisa.

Tatizo la usafiri kwa wanafunzi wanaotoka Buguruni hadi Ubungo ni tofauti na kwa mwanafunzi anayetoka Buguruni hadi Chanika hawa wa chanika wanatumia mabasi zaidi ya moja na kulipa nauli kubwa, lakini mwanafunzi akiwa na kitambulisho hiki ataweza kupanda mabasi ya UDA hata matatu kwa gharama ya shilingi 200 tu,” alisema Kisena.

Kisena alisema wanafunzi hawa watatumia vitambulisho hivyo wakiwa wamevaa nguo za shule hata kama ni mwishoni mwa wiki na tayari picha za wanafunzi 13,000 kutoka wilaya zote tatu zimeshapokelewa katika ofisi za UDA kwa ajili ya utengenezaji wa vitambulisho.

Alisema gharama za utengenezaji wa vitambulisho ni za aina 2 kuna vya shilingi 1000 na 4500 wanachosubiri ni jibu kutoka Serikali ya mkoa ili iweze kuchagua aina gani ya vitambulisho vitengenezwe kwani gharama ya utengenezaji wa vitambulisho siyo za UDA.

Wilaya ya Kinondoni ina jumla ya shule za Msingi 236 kati ya hizo 140 ni za Serikali ambazo zinawanafunzi 152,426 na shule binafsi 96 zenye wanafunzi 29,101. Shule za Sekondari ni 137 kati ya hizo 46 ni za Serikali na 91 ni za binafsi. Idadi ya wanafunzi katika shule zote za Serikali ni 44,621 kati ya hao wavulana ni 23,466 na wasichana ni 21,155.