Katibu Kinana Kuunguruma Tabora Mjini Leo

Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana

Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana

Na Bashir Nkoromo, Tabora

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kinatarajiwa kuuteka mji wa Tabora, wakati Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana atakapohitimisha ziara yake ya siku kumi mkoani Tabora kwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye Uwanja wa shule ya Sekondari Uyui.

Kulingana na ratiba iliyopo, kabla ya mkutano huo mkubwa utanaotarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi kutokana na kuonekana kupaniwa na wananchi wengi mjini hapa, Kinana atafanya shughuli mbalimbali za ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kutembelea miradi kadhaa ya maendeleo na kuzungumza na wananchi ili kusikiliza kero zao na kujadiliana nao njia ya kuzitatua.

Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye ameambatana na Kinana katika ziara hiyo amesema, Kinana anatarajiwa kuwasili leo asubuhi mjini Tabora akitokea wilaya mpya ya Kaliua ambako jana alikuwa katika mawendelezo wa ziara hiyo.

Amesema mapokezi ya Kinana na msafara wake kutoka kaliua yatafanyika eneo la Azimio saa nne asubuhi, na baadaye kwenda Kata ya Tumbi kuweka jiwe la msingi Ofisi ya CCM ya kata hiyo kabla ya kuendelea na safari yake kuingia Tabora mjini.

Maeneo mengine ambayo Kinana atachapa kazi leo mjini Tabora yametajwa kuwa ni Kinaia, Hospitali ya Kitete, Tambukareli, Gongoni,  Soko Kuu la Tabora na Kanyenye.

Hadi kukamilisha ziara yake Kinana atakuwa ametembelea wilaya zote sita za mkoa wa Tabora, akiwa amesafiri zaidi ya kilometa 2,000. Wilaya hizo ni, Igunga, Nzega, Uyui, Sikonge, Urambo, Kaliua na Wilaya ya Tabora.