Na Janeth Mushi, Arusha
KESI inayowakabili baadhi ya viongozi wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa inatarajiwa kutajwa Agosti 26 mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.
Aidha kesi hiyo ambayo jana ilitajwa mahakamani hapa, ambapo
imekuwa ikikwama kusikilizwa kwa maelezo ya awali kwa zaidi ya
mara mbili mahakamani hapo kutokana na baadhi ya watuhumiwa
kushindwa kufika mahakamani hapo shauri hilo lilipokuwa likitajwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Hawa Mguruta, alisema kuwa shauri hilo litatajwa Agosti mbele ya Hakimu Charles Magessa.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni na wenzake 18 wanakabiliwa na kesi ya kufanya maandamano yasiyo na kibali yaliyosababisha vifo vya watu watatu mnamo Januari 5 mwaka huu ambapo wanatetewa na wakili Method Kimomogolo na Albert Msando wakati upande wa serikali uliwakilishwa na Hellen Lwijage.
Awali Kimomogolo aliiomba mahakama hiyo kuwapatia ruhusa washitakiwa ambao ni wabunge kutohudhuria mahakamani hapo wakati huu ambapo bunge linaendelea ili waweze kuhudhuria kikao cha bunge cha kujadili bajeti kinachoendelea mjini Dodoma.
Washtakiwa hao ambao ni wabunge walioombewa ruhusa mahakamani hapo ni Freeman Mbowe mbunge wa Hai, Phillemon Ndesamburo9Moshi mjini), Godbles Lema (Arusha mjini) na Joseph Selasini (Rombo).
Aidha kabla ya Hakimu huyo kuashirisha kesi hiyo aliwakumbusha
watuhumiwa hao kuwa wanatakiwa kusingatia masharti ya dhamana waliyopewa ikiwa ni pamoja na kufika mahakamani pindi shauri lao linapotajwa na kuwaonya kuwa ambao hawatazingatia hilo kwa kutokufika mahakamani pasipo kutoa sababu mahakama hiyo itawafutia dhamana zao hadi kesi itakapomalizika.