KWA maneno ya siku hizi ni kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema ‘amelikoroga na kulinywa mwenyewe’, baada ya jana kutoa kauli ya kuudhi alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali lake visiwani humo, iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na kutoka.
Kauli iliyoonyesha kuwagawa wabunge katika mafungu mawili; wa bara na Zanzibar, ilimlazimu Jaji Werema baadaye kusimama bungeni na kuwaangukia akiwaomba radhi waliokerwa na kauli yake na pia kuliomba radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda na wananchi.
Kuondoka kwa wabunge hao kulitokana na mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mbarouk Mohamed kutokana na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habibu Mnyaa aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15.
Mnyaa alisema Wizara ya Katiba na Sheria ni muhimu lakini imekuwa ndiyo ya kwanza kuvunja sheria na haki za binadamu na akataka ufafanuzi.
Hata hivyo, aliposimama kujibu swali hilo, Jaji Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar na siyo katika Bunge la Jamhuri kwa kuwa si kila kitu kitaulizwa ndani ya Bunge hilo.
“Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu,” alisema Werema.
Mara baada ya Bunge kurejea, Mbarouk aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa kauli hiyo kwamba ilikuwa ya kibaguzi.
“Mheshimiwa Spika, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Alisema ubaguzi huo umewabagua wabunge ambao wamekula kiapo cha kulitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano na unaonyesha namna ambavyo Wazanzibari wanabaguliwa.
“Mheshimiwa Spika, yanapofanyika mambo kama hayo na wewe mwenyewe uko hapa unaona ni sawa na kubariki jambo hilo, huu ni ubaguzi unaoufanya wewe kwa kuwa lilifanyika ukiona bila hata ya kukemea,” alisema Mbarouk.
Hata hivyo, Spika alipinga na kusema: “Hakuna mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe umevunja sheria kwani hata nilipokuambia kaa chini umeendelea kuzungumza, tunaendelea…. Katibu (akimtaka Katibu wa Bunge kutoa mwelekeo wa shughuli iliyokuwa inafuata ambayo ilikuwa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).”
Baada ya kauli ya Spika, wabunge wa Zanzibar walihamasishana na kuamua kutoka nje kwa wakati mmoja na huku wenzao wa upinzani wakiendelea kutafakari cha kufanya. Wakati huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alikuwa akisoma hotuba yake. Muda mfupi baadaye, wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi nao walitoka na katika viti vya upinzani, alibaki John Cheyo wa UDP peke yake.
Baada ya kutoka
Akizungumza nje ya Viwanja vya Bunge, Mbarouk alisema wametoka kwa sababu Spika na Jaji Werema wamewadharau. “Hatutarejea ndani ya Bunge hadi hapo watakapotuomba radhi, wasipotuomba radhi hatutarejea bungeni,” alisema Mbarouk.
Hata hivyo, wakiwa nje ya Ukumbi wa Bunge, mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed aliwafuata na kuwaeleza kuwa amezungumza na Werema na amekubali kuomba radhi kwa wabunge na Watanzania.
“Ndugu zangu nimeongea na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amekubali kuomba radhi,” alisema Hamad Rashid jambo ambalo liliungwa mkono na wabunge wa CUF waliokuwa wamekaa katika makundi katika Viwanja vya Bunge.
Hata hivyo, wabunge hao baada ya muda wa dakika 15, walikwenda katika kikao cha dharura kwenye Ukumbi wa Kambi ya Upinzani ambako pamoja na mambo mengine, walijadiliana kusudio la kumuona Spika Makinda kumweleza mambo yasiyowaridhisha.
Werema aomba radhi
Muda mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa, Jaji Werema alisimama na kusema: “Kwa imani yangu, ninaamini kila binadamu ana nyongo, isipokuwa watu wawili… Yesu Kristo na Mtume Muhammad (SAW), ndiyo pekee ambao hawakuwa na nyongo. Naomba maneno yangu yafutwe katika kumbukumbu za Bunge hili.
“Mimi ni Jaji kwa taaluma na kwa nafasi yangu nimekosea kwa kutoa maneno hayo. Nimetambua kosa langu na naomba radhi… kwanza kwako Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rajab Mbarouk, Mheshimiwa Injinia Habib Mnyaa, Bunge hili na Watanzania kwa jumla.”
KULIKOROGA
“Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi lakini hapa si mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye vikao vyao hapa sisi hatuna majibu.”
KULINYWA
“Mimi ni Jaji kwa taaluma na kwa nafasi yangu nimekosea kwa kutoa maneno hayo. Nimetambua kosa langu na naomba radhi… kwanza kwako Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rajab Mbarouk, Mheshimiwa Injinia Habib Mnyaa, Bunge hili na Watanzania kwa jumla.”
CHANZO; Mwananchi