Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi kisiwani Pemba kushirikiana na serikali katika jitihada za kupambana na wanaosafirisha karafuu kwa njia ya magendo.
Amesema serikali imepanga kutumia sh. bilioni 36 kwa ajili ya kununua karafuu kutoka kwa wakulima wa visiwa vya Unguja na Pemba msimu huu, na kuongeza iwapo juhudi za makusudi hazitofanywa kupambana na wanaojihusisha na magendo ya karafu, si wananchi wala serikali watafaidika na fedha hizo.
Akizungumza na wananchi wa Mkanyageni mara baada ya uzinduzi wa uchumaji wa zao la karafuu msimu huu huko katika uwanja wa mpira wa Black Wizard , Dk. Shein amesema serikali imejipanga vizuri katika kupambana na wanaojihusisha na magendo ya karafuu, lakini kazi hiyo inaweza kufanyika vizuri zaidi kwa kuwashirikisha wananchi na viongozi kuanzia katika ngazi ya shehia hadi Mkoa kwani wanaofanya biashara hiyo haramu wanafahamika miongoni mwa wanannchi.
“Sisi serikalini tumejiandaa vizuri kupambana na wanaojihusisha na magendo ya karafuu, ni watu wanaojulikana, wapo wenye kujaribu kushindana na serikali, hatumuogopi mtu na hatutamuonea haya mtu yeyote” alisema Dk. Shein.
Alisema mwishoni mwa mwezi wa Februari mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya maamuzi makubwa kuhusiana na kuliendeleza zao la karafuu ambapo ilikubaliwa kwenye Baraza la Mapinduzi kwamba zao la karafuu halitobinafsishwa na badala yake serikali itaangalia dosari zilizopelekea upungufu wa uvunaji wa karafuu kwa lengo la kurekebisha dosari hizo ili hatimaye kulirejesha zao hilo katika kiwango chake cha asili cha uvunaji.
Uamuzi mwengine wa serikali katika kuliendeleza zao la karafuu ni kupandisha bei kutoka Tsh. 4500 mwaka uliopita hadi kufikia tsh. 18,000 kwa pishi mwaka huu, kiasi ambacho hakijawahi kupandishwa katika historia ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema pamoja na hatua hizo, serikali itaendelea kupandisha bei ya karafuu kila bei ya zao hilo itakavyokuwa inapanda kwenye soko la dunia, na kwamba bei hiyo haitopunguzwa hata kama bei itaanguka kwenye soko la dunia.
“Tumeweka msimamo kwamba tutapandisha bei ya karafuu kulingana na mwenendo wa bei katika soko la dunia, na hatutashusha bei hata kama bei itaanguka kwenye soko la dunia” alisema Rais wa Zanzibar.
Ameongeza kuwa katika hatua nyengine ya kuimarisha zao la karafuu, serikali inakusudia kutoa miche zaidi ya 500000 ya mikarafuu bila ya malipo kwa wakulima wa mikarafuu na kuwaajiri wataalamu wa kilimo watakaosambazwa kwenye maeneo yote ya kilimo Unguja na Pemba kusaidiana na wakulima wa mazao mbali mbali ikiwa ni pamoja na upandaji wa mikarafuu.
Dk. Shein amesema hatua zimeanza za kutengeneza alama maalum “branding” itahayotumika kwa karafuu za Zanzibar na hatimiki hatua ambayo litasaidia sana kuitangaza na kuipa hadhi karafuu ya Zanzibar ndani na nje ya nchi. Aidha, alama hiyo kwa upande mwengine itasaidia kushusha hadhi ya karafuu zinazouzwa kwa njia ya magendo ambazo hazitakuwa na alama hiyo.
Amesema jitihada hizo zote zinalenga kuinua maisha ya mkulima wa zao la karafuu na pia kulirejeshea hadhi zao hilo ambalo bado ndio mhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar hadi sasa, licha ya juhudi mbali mbali ambazo serikali imekuwa ikichukua kuanzisha mazao mengine ya biashara.
Amewataka wananchi kwenye maeneo yao yote kuhakikisha kuwa karafuu zao zote zinauzwa kwenye vituo vya serikali vya ZSTC kwani amesema kufanya hivyo ndiko kutakakoisaidia serikali kupata mapato yanayotokana na karafuu na hivyo kusaidia katika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Akizungumzia kuhusu uwezo wa serikali kumudu kununua karafuu za wakulima, Rais wa Zanzibar amewahakikishia wananchi kwamba serikali imetenga fedha za kutosha za kununulia karafuu katika msimu mzima wa karafuu kwa bei iliyotangazwa na hata kama itapandishwa zaidi.
Wakati huo huo Dk. Shein ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa mara baada ya kumaliza mkutano huo wa hadhara ambao ulihudhuriwa na mamia ya wananchi alitembelea Tawi la CCM lililopo Shidi, Jimbo la Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba.