Na Magreth Kinabo – Maelezo
RAIS Jakaya Kikwete amewataka Wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa wanasimamia Mpango Mkakati ulioboreshwa wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza vifo vya Uzazi vya wakinamama na watoto hususan wachanga ili kutimiza malengo ya milenia namba nne na tano ifikapo mwaka 2015.
Aidha Rais Kikwete aliagiza viongozi wa mapango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kuliingiza suala la afya katika mpango huo. Changamoto hiyo imetolewa na Rais Kikwete kabla ya kuzindua mpango huo, ulioenda sambamba na uzinduzi wa kadi ya ufuatiliaji(scorecard) ambayo itakuwa inaonesha tathimini na ya maendeleo na mkakati huo kwa kila mkoa na wilaya.
Rais Kikwete aliwataka wakuu hao na watendaji wao kutoa ripoti ya kadi ya ufuatiliaji kila baada ya miezi minne. Kadi hiyo, ambayo itakuwa na taarifa ya maendeleao ya kupunguza vifo vya watoto wachanga, chini ya miaka mitano na wakinawajawazito.
Uzinduzi huo, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu J.K. Nyerere jijini Dares Salaam.
Alisema vifo vya uzazi vya wakina mama vimepungua kutoka 578 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2005 na kufikia vifo 454 kwa vizazi hai 100,000 kwa sasa, wakati lengo la milenia ni vifo 193 kwa vizazi hai 100,000.
“Bado tuna safari ndefu ninawataka wakuu wa mikoa na wilaya kuchulikia jambo hili kwa umakini na kulipa kipaumbele kwani jukumu hili si la waganga wakuu wa mikoa au wilaya na mimi nitakuwa ninafuatilia kwa kuwa jambo hili, lipo mikononi mwangu. Ninataka kulifuatialia kabla sijamaliza kipindi cha uongozi wangu,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa vifo hivyo vya wakina mama na watoto hutokea lakini havifatiliwi ndio maana inakuwa vigumu kubaini njia za kuvipunguza. “Baya zaidi wanakufa kwa sababu zinazoweza kuzuilika, kadi ya ufuatiliaji ikifuatiliwa na wakuu wa mikoa itasaidia kupunguza vifo,” alisisitiza.
Alisema ikiwa watoto waliochini ya miaka mitano na wakinamama wajawazito watazingatia masuala ya lishe bora kwa kipindi cha siku 1000 pia itasaidia kupunguza vifo hivyo. Huku akisema vyakula hivyo vipo majumbani kinachohitajika ni elimu.
Aliwataka wakimama kuzingatia uzazi wa mpango (nyota ya kijani) ili kusaidia kupunguza tatizo hilo, pia kushirikisha wanaume juu ya jambo hilo. Rais Kikwete pia alisema asilimia 51 ya wakina wanaojifungua huhudumiwa na watalaamu wenye ujuzi, wakati malengo ya milinea ni asilimia 80, hivyo bado kuna changamoto ya asilimia 29.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, alisema kwa kipindi cha mwaka huu wanampango wa kuajiri watalaamu hao 11,021. Alisema Tanzania imefanikiwa kutimiza lengo la milinea namba nne kabla ya wakati kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa kiwango cha 54 kwa watoto wanaozaliwa 1000, kutoka 165 kwa wataoto wanaozaliwa 1000 mwaka 1990. Alizitaja nchi nyingine zilizofanikiwa ni Rwanda, Malawi, Ethiopia Rwanda na Malawi.
Naye mwakilishi wa wakuu hao, Dk. Christine Ishengoma alisema uwajibikaji wa viongozi na watendaji ni jambo la muhimu katika kutekeleza mpango huo, hivyo suala hilo linawezekana. Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Dk. Deo Mutasiwa alisema sheria ndogondogo zinatengenezwa ili kuwezesha mpango huo kufikia lengo.
Dk. Mutasiwa alizitaka halimashauri kutumia vyanzo vyake vya mapato ya ndani kwa asilimia 60 kuwekeza katika masuala ya afya, elimu maji na barabara za vijijini. Alisema hivi sasa wako katika mchakato wa kupata kibali cha kuwaezesha watoa huduma wa afya wanaomba nafasi za kazi kufanyia kazi maeneo wanayotoka.