TAMKO LA WANAHARAKATI WA NGAZI YA JAMII NA WASHIRIKI WA GDSS DHIDI YA MWENENDO WA BUNGE LA KATIBA LILILOPITA.
Wanaharakati wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na TGNP Mtandao tunatoa tamko hili baada ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa bunge la Katiba lililomaliza hivi karibuni. Tumeshtushwa sana na namna bunge hili lilivyoendeshwa na kugubikwa na kasoro mbali mbali ambazo zisipochukuliwa hatua madhubuti kuna uwezekano wa kutopata Katiba au kupata Katiba ambayo haitokani na mapendekezo au maoni ya wananchi walio wengi.
Bunge hili liligubikwa na Kauli za kuudhi, matusi, kauli za kibaguzi, dharau za Kijinsia, vitisho na siasa chafu na ushabiki wa kisiasa unatokana na utashi wa vyama. Hali hii ilipelekea masuala ya msingi yanayogusa ustawi wa taifa kutojadiliwa na kupelekea baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba kususia bunge hilo.
Wakati Bunge hili limetumia billion 27 kwa siku 67 walizokaa kujadili kanuni za bunge maalum la katiba na sura mbili za rasimu ya katiba, ni dhahiri limewanyima watanzania fursa ya masuala ya msingi yanayowahusu kutojadiliwa. Hali hii imewaweka watanzania wengi njia panda kwani hadi sasa hawajafanya kazi waliotumwa. Wakati huo huo kazi waliofanya iko chini ya matarajio ya wananchilakini wametumia pesa ambazo zingeweza kuelekezwa katika huduma za msingi za wananchi kama vile maji, afya, elimu na miundombinu mibovu.
Pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuonesha nia njema ya kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya hapa Tanzania, nia hiyo haionekani kuwa ndani ya wanasiasa kwa ujumla wake. Kwa vitendo na maneno ya watendaji waandamizi wa serikali ya Tanzania, Wanaharakati wa ngazi ya jamii na wana GDSS tunachelea kuamini kuwa ipo nia ya dhati na ya kweli ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inapata Katiba Mpya inayotokana na maoni ya Watanzania wenyewe. Kwa mwelekeo wa mijadala ya hivi karibuni ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba pamoja na serikalini, nia ya watawala inaonekana kuwa ni kutaka kufanya mabadiliko madogo madogo katika Katiba ya sasa na kuacha kila kitu kama kilivyo. Kwa mtazamo wetu,hiyo inapingana na nia na kiu ya watanzania walio wengi kuona kuwa Mchakato wa Kuandika Katiba Mpya unaleta mapinduzi ya Kikatiba yatakayokuwa chachu ya nchi yetu kuongozwa kwa misingi ya uwazi, uhuru, demokrasia na kuheshimu utu wa mtu na haki za binadamu.
Mapungufu katika sheria inayoongoza Mchakato huu ni makubwa kiasi kwamba utata wa mchakato mzima ni wa Kisheria. Kwa mfano, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilivyo sasa inashindwa kutoa mwelekeo thabiti wa nini kifanyike inapofikia hali ya sintofahamu na mkanganyiko wa mchakato kama ilivyo sasa. Mianya hiyo ya Kisheria imepelekea utata katika utungaji Kanuni za Bunge Maalum la Katiba hadi kuleta mkanganyiko na kufanya Bunge kutofikia muafaka katika maeneo kadhaa ikiwemo aina ya Kamati ya Utendaji, kura katika kupitisha vifungu vya rasimu, idadi inayohitajika katika kupitisha jambo ndani ya Bunge Maalum pamoja na mambo mengine kadhaa.
Hata malalamiko yaliyopo hivi sasa juu ya baadhi ya makundi kutokuwa na uwakilishi ndani ya Bunge Maalum la Katiba ni suala lenye mizizi yake kaika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Suala hii limeleta hisia kuwa liliwekwa hivyo makusudi kisheria ili CCM iwe na wajumbe wengi kuliko makundi mengine ndani ya Bunge Maalum la Katiba na hivyo kupitisha vifungu vya Katiba kwa urahisi bila kuhitaji maridhiano na pande zenye mawazo tofauti.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 ya imempa Rais madaraka makubwa sana katika hatua zote sita za mchakato wa Katiba Mpya,Rais ana sauti na mamlaka makubwa sana ya kufanya maamuzi kuanzia kutangaza kuanza/kusitishwa kwa mchakato, kutungwa na kurekebishwa kwa sheria, uteuzi, uendeshaji na uvunjaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum laKatiba, uzinduzi, uendeshaji na uvunjaji wa Bunge la Katiba na usimamizi wa mchakato mzima wa Katiba. Hali hii imepelekea Rais ambae pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kuingilia mchakato huu kwa kofia ya chama. Kwa mfano maamuzi yaliofikiwa na Kamati kuu ya chama cha mapinduzi hivi karibuni hayaonyeshi kama CCM ina nia njema na mchakato huu wa katiba kwa sababu……………
Ushiriki wa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano katika bunge maalum la katiba kumewanyima nafasi wananchi kukutana na wawakilishi wao ili kuwasilisha masuala yao katika bunge la bajeti linaloendelea, hali hii imepelekea watanzania kutowakilishwa vyema kwenye bunge hili la bajeti na kukosa sauti za wananchi.
Kutokana na tuliyoyaeleza hapo juu tunadai yafuatayo:
i. Mchakato wa maridhiano kati ya pande mbili zinazosigana (UKAWA na Tanzania Kwanza) ufanyike haraka ili kuweza kunusuru mchakato na bunge la katiba.
ii. Kutokana na bunge maalum kutumia fedha nyingi kinyume na ilivyotarajiwa na kazi walioifanya ipo chini ya matarajio ya watanzania, tunadai awamu ya pili ya bunge hili matumizi yapungue ili fedha zielekezwe katika kugharamia masuala ya maendeleo.
iii. Kwakua wananchi walitoa maoni yao na ndio msingi wa chimbuko la madaraka na mamlaka yote ya nchi tunadai maoni ya wananchi yaliopo katika rasimu ya katiba, yaheshimiwe.
iv. Dharau, ubabe, vijembe, vitisho, matusi, kashfa na ubaguzi wa kijinsia unaokuzwa na kulelewa na kanuni za bunge maalum la katiba, tunadai ziundiwe kanuni mpya kwa ajili ya kuondoa na kukemea vitendo hivyo.
v. Tunalaani malumbano yasio na tija yenye lengo la kupoteza muda ili wajumbe wa bunge maalum la Katiba waongezewe siku na posho.
vi. Bunge la katiba limejipa madaraka makubwa yakubadili rasimu ambayo imebeba maoni ya wananchi. Tunadai maoni yaliopo katika rasimu ya katiba ilioandaliwa na tume ya Warioba yaheshimiwe.
vii. Kama hayo yote hayakuheshimiwa na kuzingatiwa, tunadai bunge hili la Katiba livunjwe na kuundwa kwa bunge jipya la Katiba litakalobeba uwakilishi wa wananchi wenyewe hasa makundi ya walio pembezoni.
Imetolewa na kusainiwa kwa niaba ya washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) na wanaharakati wa ngazi ya jamii
MAmina Mcheka Badi Darusi
……………………… …………………….
Mwenyekiti Katibu
Tarehe 14, Mei 2014