Mbunge CCM Adai Serikali ya CCM Inaendeshwa Kisanii

Alphaxard Kangi Lugola

Alphaxard Kangi Lugola

MBUNGE machachari wa Mwibara, Alphaxard Kangi Lugola, amedai kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii. Lugola ambaye katika Bunge lililopita aliwaongoza wabunge wenzake kuichachafya Serikali hadi mawaziri wanne kujiuzulu nyadhifa zao, jana aligeuka tena mwiba kwa Serikali ya CCM. Akichangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Lugola alisema anashangaa Waziri mwenye dhamana, Christopher Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blabla.

Pia alimgeukia naibu wa wizara hiyo, Godfrey Zambi na kumwambia kuwa amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma bungeni akipaza sauti, lakini baada ya kupata madaraka amewageuka na kushirikiana na waziri. Akichangia kwa hisia kali, Lugola alihoji inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki ofisini kama Waziri.

“Waziri huyuhuyu ndiye anayezindua mbegu aina ya Chutoni ambayo haioti, bado ni Waziri. Waziri huyu huyu analipa ruzuku mbegu ya pamba isiyoota bado ni Waziri,” alisema Lugola.

Lugola alihoji kama Mchina aliyekuwa akijenga daraja la Kilombero alijiua kwa sababu tu ya kuhofia kupigwa risasi atakaporudi kwao, hata Waziri Chizza alipaswa awe ameiacha kazi hiyo.

“Simshauri waziri ajiue, lakini kwa vitendo vyote hivi waziri huyu angekuwa ameacha wizara hii na kupumzika na kufanya kazi nyingine mbadala,” alisema Lugola huku akipigiwa makofi.

Lugola alikumbushia Chizza alikuwa ni miongoni mwa mawaziri waliotajwa kuwa ni mizigo na kusema mambo yanayofanywa na wizara hiyo yatakigharimu Chama Cha Mapinduzi. Mbunge huyo alibainisha kuwa, katika hotuba yake mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha mfuko wa kinga ya pamba ili kuwasaidia wakulima.

Hata hivyo, alisema katika hotuba ya Waziri Mkuu juzi, hakuna sehemu aliyozungumzia mfuko huo wala Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika hotuba yake ya mwaka huu, naye hajazungumzia mfuko huo.

“Hivi nchi hii tunaiendesha kwa usanii mpaka lini? Usanii juu ya usanii… Hatuwezi kuwadanganya wananchi kwa kiwango hiki. Itakuwaje mimi mbunge niunge mkono bajeti ya namna hii?” alihoji.

Alimgeukia Zambi na kumweleza kuwa aliwahi kumtahadharisha kuwa atakapokuja na bajeti yake ahakikishe anampa majibu ya asilimia 20 ya malipo waliyoahidiwa wakulima waliotumia mbegu ya chutoni.

“Uniambie asilimia 20 ya malipo ya wakulima ambayo waliahidiwa kwamba wakitumia chutoni walipwe kama sehemu ya malipo yao, lakini hili halimo kwenye bajeti,” alisema na kuongeza:

“Hakuna lolote humu ni blabla tu… Mheshimiwa Zambi wewe ulikuwa ‘backbencher’ (kiti cha nyuma) kama mimi ulikuwa unapiga muziki kama kasuku juu ya wizara hii, leo unashirikiana na waziri wako unakuja na vitu ambavyo havina majibu, maana yake nini?”

Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema wakati Zambi akiwa mbunge, alikuwa msitari wa mbele kupinga matumizi ya mbolea ya minjingu na kumtaka aeleze kama bado ana msimamo huo. Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), aliwashukia wakuu wa mikoa ya Simiyu na Geita kuwa ni chanzo cha tatizo kwa wakulima wa pamba.

Mbali na hilo, amemtaka Balozi wa Uingereza nchini ajitokeze kueleza misaada inayotolewa na nchi yake inavyotumiwa kwenye sekta ya pamba kwani imekuwa ni sehemu ya ubabaishaji kwa kuendeshwa semina zisizo na maana. Shibuda alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia maoni kwenye hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2014/15.

Aliwatuhumu wakuu hao kuwa walimpeleka Waziri Mkuu katika kampuni ya Kiotoni wakamdanganya kuwa mbegu hizo ni nzuri, lakini kumbe hazikuwa zimefanyiwa utafiti wa kina na kuwasababishia hasara kubwa wakulima. Shibuda alisema mbegu za kiotoni zina udhalimu mkubwa na hazina tija yoyote kwa wakulima lakini kila siku wakuu wa mikoa na wilaya wanazipigia debe licha ya kuwa wanatambua kwamba wakulima wanaumizwa. Magdalena Sakaya aliifananisha Serikali kuwa ni sawa na sikio la kufa kwa kuwa kila wakati imeshindwa kuwa na majibu ya ukombozi kwa wakulima wa Tanzania ambao ndio wapigakura wao.

Mbunge wa Kasulu, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) aliwapongeza wabunge wa CCM wanaoonyesha ujasiri wa kuisema Serikali yao kuwa inaendesha mambo kisanii na hivyo kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo.

“Serikali imekuwa ikidanganya katika kutatua matatizo ya wananchi ndiyo maana tunaona ni Serikali ya maigizo… Ukisoma hotuba ya bajeti hapa haijibu matatizo ya wananchi,” alisema.

Wakati wabunge hao wakiiponda bajeti hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Serikali, kueleza ni lini na vipi wakulima walioathirika na mbegu feki watafidiwa. Msemaji wa Kambi hiyo wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili, alisema tayari wakulima wameshapata hasara na bado wako wanaoendelea kuathirika na tatizo la mbegu kutoota.

CHANZO; Mwananchi.