Wabunge wa Chadema watolewa bungeni


Askari wa Bunge wakiwasindikiza wabunge wa CHADEMA Tundu Lissu (kulia) , Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) na Godbless Lema (wa pili kushoto) kuondoka nje ya viwanja vya Bunge mara baada ya Naibu Spika, Job Ndugai (hayupo pichani) kuwaamuru watoke ndani ya Bunge kwa kile kudai wamevunja kanuni za Bunge. Wa pili kulia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika akiwasindikiza.

Dodoma.

WABUNGE watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema (Arusha Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Mchungaji Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini jana wamefukuzwa bungeni.

Job Ndugai (Mbunge wa Kongwa) na Naibu Spika alitoa uamuzi huo mjini hapa majira ya saa 6 mchana ikiwa ni muda mfupi baada ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Lema, kusoma taarifa mbadala ya bajeti ya wizara hiyo.

Wakati Lema akiendelea, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, aliomba utaratibu kwa Naibu Spika kwa kile kutoridhishwa na kauli za Lema kwenye hotuba yake.

Lukuvi alisema; licha ya kwamba kila chama kina uhuru wa kueleza mtazamo juu ya wizara husika, lakini kinachowasilishwa na Lema hakikubaliki kwani hotuba yake imejaa maneno ya uchochezi.

Lukuvi alisema hata kanuni za bunge haziruhusu wabunge kuzungumza mambo wasiyokuwa na uhakika nayo. “Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima zote za kiti chako na kwa maelekezo ambayo umekuwa ukitoa bungeni, Kanuni ya 64 imevunjwa na Mheshimiwa Lema wakati akiwasilisha hotuba yake hapa.

“Kanuni hii leo imevunjwa na hotuba nzima, kama ulivyotutangazia asubuhi, sisi tumekuwa wavumilivu sana, lakini Watanzania wenyewe watapima na kwa uvumilivu tulionao tulitaka yote yasikike ili Watanzania wenyewe wapime.

“Hivi Mheshimiwa Naibu Spika, mbunge aliyechaguliwa na wapiga kura anaweza kusema vile!, kuna maneno hapa yametumika kama Tanzania siyo nchi ya haki na heri kuwa na vita,” alisema Lukuvi.

Hata hivyo akiendelea zilianza kelele kutoka upande walikokaa wabunge wa CHADEMA, hivyo Naibu Spika kuingilia na kumpa nafasi Lukuvi kuendelea kueleza. “Polisi leo wanaagizwa wakiuke maagizo ya makamanda wao na hata kama kuna maandamano wasiende kuyalinda, tunaambiwa uchaguzi wa Arusha ni batili, kwa kweli hotuba hii ya Lema imejaa uchochezi mkubwa, yaani kuanzia mwanzo mpaka mwisho wake…

Baadaye Lissu alisimama kuomba mwongozo; “hivi huyu ameomba utaratibu au anatoa hotuba?”. Lissu alipokuwa akiendelea, Lema akasimama na kuomba naye mwongozo. Kabla hajazungumza, Naibu Spika akasimama, Mchungaji Msigwa naye akasimama na kusema; “huu ni upendeleo wa hali ya juu, huyu amesimama kuomba utaratibu na sasa anahutubia, maana yake nini?”.

Ndipo Naibu Spika akasimama na kuendelea; “Kwa kuwa nimesema tangu asubuhi kwamba hakuna kuzungumza bila ruhusa…kuna watu watatu nimewaona wakizungumza bila kufuata utaratibu, sasa watu hao watatolewa nje ya Bunge sasa hivi.

“Mtu wa kwanza ni Tundu Lissu, mtu wa pili ni Mchungaji Msigwa na wa tatu ni Lema, nawaomba watoke nje sasa hivi na nitahakikisha wanasindikizwa hadi nje ya geti la Bunge kabisa,” alisema Naibu Spika na wabunge hao kuondolewa bungeni.