Chato,
MAOFISA wanne kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Kagera wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutafuna fedha za pembejeo za kilimo zilizotakiwa kupewa wakulima. Kati ya waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo yumo Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Robert Matungwa pamoja na wakala wa usambazaji pembejeo.
Watuhumiwa wote walisomewa mashtaka hayo jana mjini hapa na mwendesha mashtaka wa polisi wilayani hapa, Rashid Mkwasi mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Chato, Khassani Khoja.
Mkwasi alidai watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Oktoba, 2010 na Februari mwaka huu, ambapo kwa nyakati tofauti walikula njama na kujipatia fedha kinyume cha sheria, na kuiba sh. bilioni 1.3.
Mkwasi aliwataja watuhumiwa hao ni Dk. Phares Tongola (56) Ofisa Kilimo na Mifugo wa Wilaya ya Chato, Elihuruma Delingo (51) ambaye ni Ofisa Kilimo Wilaya na Jonas Rwejuna Suzzo (59) Bwana shamba wa halmashauri ya Chato.
Alidai wanadaiwa kuiba fedha za Serikali zilizotolewa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kupitia Halmashauri ya Chato ikiwa ni ruzuku ya kununulia mbolea na mbegu kwa wakulima.
Akisomewa mashtaka mwanasheria wa halmashauri hiyo, Matungwa, anadaiwa kutenda makosa matatu likiwemo la matumizi mabaya ya ofisi, kufanya udanganyifu ilhali akijua ni kosa pamoja na kuandaa barua kumb. CDC/MKTB/3/2/17 ya mwaka 2010 ya usambazaji pembejeo za kilimo bila idhini ya Bodi ya Manunuzi.
Aidha amewataja watuhumiwa wengine ni Bitus Raurens (40) aliyekuwa wakala mkuu wa mawakala watano, ambao bado nao wanatafutwa na polisi kwa kula njama na kujipatia fedha sh. milioni 349.5 kinyume cha sheria na jumla kukabiliwa na makosa 16.
Wengine ni Christopher Mabuba (36) Mtendaji wa Kijiji cha Bwanga (makosa 6), Paul Madema (49) Mtendaji wa Kijiji cha Kakola (makosa 4). Watuhumiwa wengine ni Julius Kulusanga, Cosmas Kazimili (51) Mtendaji wa Kijiji cha Bwera, Emmanuel Sosoka, Mtendaji Kijiji cha Kisesa na Leah Makingo wote wakiwa na makosa mawili ya kula njama na kujipatia fedha kwa njia isiohalali.
Wamo pia Dicksoni Mryashinge (53) aliyekuwa Katibu wa Kamati ya pembejeo ya Kijiji cha Bwanga, na Salvatory Bakilabe (37) Mtendaji wa Kijiji cha Bukiliguru, kila mmoja akiwa na makosa mawili. Watuhumiwa wanane kwa kushirikiana na wakala huyo wanadaiwa kuiba sh. biloni 1.3 hali iliyosababisha wakulima kukosa pembejeo zilizotolewa na Serikali.