JK, Waziri Mkuu wa China Wazungumzia Mahusiano

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Mhe. Li Keqiang pembeni ya Mkutano wa Uchumi Duniani kwa bara la Afrika  jijini Abuja, Nigeria, Mei 7, 2014.

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa China Mhe. Li Keqiang pembeni ya Mkutano wa Uchumi Duniani kwa bara la Afrika  jijini Abuja, Nigeria, Mei 7, 2014.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mei 7, 2014 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Li Keqiang.

Katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Transcorp Hilton ya mjini Abuja nchini Nigeria ambako wote wawili wamefikia wakati wanashiriki katika Kongamano la Uchumi Duniani Afrika (World Economic Forum – Africa), viongozi hao wawili wamezungumzia, kimsingi, mambo yanayohusu uhusiano wa Tanzania na China.

Katika mkutano huo, Rais Kikwete amemwomba Li Keqiang kuisaidia Tanzania kuboresha mfumo wake wa kutunza na kuhifadhi nafaka kutokana na ongezeko kubwa za uzalishaji wa nafaka, ambao unatokana na kukua kwa kilimo cha Tanzania.

Waziri Mkuu Li Keqiang amekubali ombi hilo la Tanzania kwa kumweleza Rais Kikwete Waziri wa Serikali ya China ambaye atasimamia kutekelezwa kwa mradi huo mkubwa kutokana na ongezeko kubwa la nafaka katika kilimo cha Tanzania.

Rais Kikwete pia amemwomba Waziri Mkuu huyo wa China kusaidia kuhakikisha kuwa kazi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo inaanza mapema iwezekanavyo, ombi ambalo Waziri Mkuu Li Keqiang amelikubali.

Rais Kikwete pia ameipongeza China kwa dhana yake iliyotangazwa karibuni ya 4-6-1 ambako kuna misingi minne, maeneo sita ya kipaumbele na eneo moja la mwelekeo kama msingi mkuu wa Siasa za Nje za Jamhuri ya Watu wa China.

Rais Kikwete pia ameisifu China kwa kusaidia maendeleo ya Afrika kwa kutoa misaada ya maendeleo, kuwekeza na kufanya biashara na Bara la Afrika na pia kuiwezesha Afrika kupata teknolojia ya kisasa kutoka China.

Aidha, Rais Kikwete ameishukuru China kuwekeza katika uchumi wa Tanzania, akisema kuwa China ni moja ya wawekezaji wakuu katika uchumi wa Tanzania kwa kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5.

“Tunashukuru sana kwa uwekezaji wa kila aina, wa mwisho mkubwa ikiwa ni kutupatia mkopo wa kiasi cha dola milioni 1.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam,” amesema Rais Kikwete na kuongeza kumshukuru Waziri Mkuu kwa misaada ya kijeshi ambayo Tanzania inaipata kwa China. “Nchi yetu inalindika vizuri zaidi kwa sababu ya misaada yenu.”

Naye Waziri Mkuu Li Keqiang ameipongeza Tanzania kwa kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na pia ameonyesha furaha yake kuona maendeleo ya kiuchumi ambayo Tanzania inaendelea kuyapata.

Alisema kuwa urafiki wa China na Tanzania siku zote umekuwa msingi mkuu wa mahusiano ya China na Afrika na hali hiyo itaendelea kuwa ukweli wa mahusiano baina ya China, Afrika na Tanzania.