Hotuba ya Makamu wa Rais, Dk Bilal Katika Ibada ya Kusimikwa Askofu Mteule Alen Siso
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KATIKA IBADA YA KUSIMIKWA ASKOFU MTEULE ALEN SISO WA KANISA LA METHODIST TANZANIA- JIMBO TEULE LA MASHARIKI NA PWANI, DAR ES SALAAM, TAREHE 3.5.2014
Mhe. Said Meck Sadiki, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Baba Dkt. Mathew Byamungu , Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania ;
Alen Siso, Askofu wa Jimbo Teule la Mashariki na Pwani;
Mhe. Jordan Rugimbana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni;
Maaskofu na Wakuu wa Madhehebu mbalimbali mliopo;
Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa mliopo hapa;
Wawakilishi wa Mashirika na Wahisani mbalimbali;
Ndugu Waandishi wa Habari;
Waumini wote mliohudhuria;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Bwana Yesu asifiwe!
Aawali ya yote, tuna kila sababu kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema , kwa kutupa uzima na kutuwezesha kukusanyika hapa siku leo. Tuliopata kibali hiki, ni upendeleo wa aina yake, wapo wenzetu wengi, wameshindwa kuiona siku ya leo, wengine wamelala hospitalini wakipigania uhai. Sisi tuliopata nafasi hii, tuna kila sababu, kumrudishia Mungu sifa na utukufu.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Kabla sijaendelea, napenda niseme neno moja; Nimekuwa na bahati kubwa kusimama chini ya dari ya Kanisa la Methodist Tanzania. Nakumbuka ni mwaka jana, Aprili 27, mlinialika katika Harambe na Ibada Maalumu ya kumshukuru Mungu, kwenye Kanisa la Methodist Tanzania, pale Msasani. Leo hii mmenialika tena katika tukio hili la kihistoria, la kusimikwa Askofu Mteule Alen Siso. Nawashukuru sana, kwa moyo wa upendo na heshima kubwa mnayonipa. Sina maneno mazito ya kushukuru, zaidi ya kusema ; Bwana azidi kuwatunza na kuwapigania !
Nichukue fursa hii kipekee, kukushukuru wewe binafsi Baba Askofu Mkuu Dkt. Byamungu, Watendaji wa Jimbo Teule la Mashariki na Pwani, na Uongozi mzima wa Kanisa la Methodist Tanzania, kwa mwaliko wenu wa leo. Nimeupokea kwa moyo mweupe, na mikono miwili. Asanteni sana.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu waumini;
Napenda nitumie nafasi hii, kulipongeza Kanisa la Methodist Tanzania, chini ya uongozi wako Baba Askofu Mkuu, Dkt. Byamungu , kwa namna mnavyoendelea kupanuka, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali, kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Kwa mujibu wa maelezo, Kanisa la Methodist Tanzania, lilianza kutoa huduma ya kiroho hapa nchini, Juni 12 mwaka 1991. Leo hii lina miaka 23 tu, lakini tumeona namna lilivyopiga hatua kubwa, kuchangia nyanja mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Ujenzi wa hospitali tano mkoani Geita, shule mkoani Arusha, uchimbaji visima virefu kwa shule na magereza katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na ujenzi wa Chuo cha Theolojia huko Dodoma na Arusha, ni baadhi tu ya mambo mengi mema, yanayofanywa na kanisa hili. Kwa niaba ya Serikali, nawapongeza kwa kazi kubwa mnayofanya. Tutaendelea kuwa karibu nanyi, kwa kila jambo mtakaloona tunapaswa kushirikiana.
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda nipongeze pia, mchango mkubwa unaotolewa na mashirika na taasisi mbalimbali za dini hapa nchini, kusaidia juhudi za Serikali kuwaletea wananchi wake maendeleo. Taasisi na mashirika ya dini, yamekuwa mstari wa mbele kujenga shule, vyuo, hospitali na huduma zingine mbalimbali za jamii. Serikali peke yake haiwezi kufanya miujiza.Tunathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika na taasisi zote za dini . Nawahakikishia kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika haya, kwa maslahi ya maendeleo ya nchi yetu.
Wito wangu kwa mashirika na taasisi za dini; Fanyeni kila linalowezekana, kuboresha zaidi huduma zenu, ili ziendane na ushindani wa zama hizi. Hakikisheni mnakuwa na shule bora za kisasa zenye vifaa vya kutosha kufundishia, kadhalika hospitali zenu ziwe za kisasa , hata visima mnavyochimba, viwe na ubora wa unaotakiwa. Nawatia shime; Kazi mnayofanya ni nzuri, endeleeni na moyo huo, na Bwana atazidi kubariki kazi za mikono yenu.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa Watanzania kudumisha amani na mshikamano wetu, ambao umekuwa tunu kubwa tangu tulipopata Uhuru. Ni juzi tu tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wetu huku nchi yetu ikiendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu. Katika hili, nawakumbusha watu wa Mungu kukesha na kuliombea Taifa letu. Si watu wote wanafurahia mafanikio haya. Wapo wanaotuombea mabaya usiku na mchana, wanataka waone siku moja tumefarakana na kupoteza mwelekeo. Naamini watu wa Mungu mkisugua goti katika hili, kamwe Shetani hatapata nafasi ya kujiinua katika Taifa letu.
Sisi katika Serikali, tutaendelea kusimamia kwa nguvu zote, dhamana kubwa mliyotupa, ya kudumisha Umoja na Mshikamano wa nchi yetu. Naamini kwa kuwa hata Mungu wetu hafurahii mafarakano na utengano, ataendelea kusimama upande wa haki kutupigania. Tutaendelea kusimamia misingi ya utawala wa bora bila kujali rangi ya mtu kabila, dini, jinsia wala eneo analotoka.
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Upendo ni sharti muhimu sana katika maisha ya kila siku ndani ya jamii. Nilipozungumza nanyi mwaka jana huko Msasani, nilizungumzia hili, Napenda kurudia tena katika hadhara hii. Nazungumzia hili kutokana na mazingira ya mpito ambayo Taifa letu, linapita kwa sasa.
Baba Askofu Mkuu, ni vigumu nchi yetu kuendelea kuwa na amani kama watu wetu hawapendani. Ni vigumu watu wetu kuendelea kukaa pamoja kama hawavumiliani. Ni vigumu nchi yetu kuendelea kuwa ya amani na utulivu, kama watu wetu hawaheshimiani. Bila Upendo na Kuvumiliana, Taifa letu litasambaratika.
Tupo katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya. Tulianzisha mchakato huu kwa nia njema ya kuwawezesha Watanzania kupata Katiba, inayoendana na mazingira ya sasa. Tofauti na ilivyotarajiwa, mchakato huu umeanza kugubikwa na malumbano huku baadhi ya Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba, wakitangaza kususa vikao. Kukosekana Upendo, ni moja ya sababu kuu ya kushindwa kuvumiliana, hata katika mijadala ya Bunge la Katiba.
Ndani ya Biblia takatifu, Kitabu cha Wakorintho wa Kwanza, mlango wa 13, mstari wa 4 hadi 8, kimezungumza vizuri sana kuhusu Upendo; nitanukuu:- “Upendo huvumilia, hufadhili, upendo hauhusudu, upendo hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu,hauhesababu mabaya, haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli, huvumilia yote, hustahimili yote, upendo haupungui neno wakati wowote… Ukiendelea mstari wa 13, unahitimisha kwa kusema:- “Basi sasa inadumu imani, tumaini , upendo haya matatu; na katika hayo, lililo kuu ni UPENDO.”
Pia Maandiko matakatifu katika Waraka wa Kwanza wa Petro Mtume, mlango wa 4, mstari wa 8 hadi 10, yanasema hivi; nitanukuu:-” Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana kwasababu upendano husitiri wingi wa dhambi. Mkaribishane ninyi kwa ninyi pasipo kunung’unika kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.”
Nawasihi waumini wa dini zote nchini, kuzidi kuombea jambo hili , ili mchato huo, ufikie hatma njema kama ilivyokusudiwa. Nawakumbusha pia Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba, watakaporejea Agosti mwaka huu, kujenga upendo miongoni mwao , wakumbuke kwamba wanawakilisha mamilioni ya Watanzania. Biblia imetuambia kuwa wakijenga upendo, Watavumiliana, hawatahesabiana mabaya, hawatapenda udhalimu na wala hawatakoseana adabu.
Baba Askofu Mkuu;
Viongozi wa dini mbalimbali mliopo;
Ndugu Waumini;
Jukumu mlilotupa la kuongoza Watanzania, haliwezi kuwa na tija, kama wananchi tunaowaongoza, hawatamjua Mungu na kufuata mafundisho yake. Watu wetu wakimjua Mungu hawatatoa wala kupokea rushwa, hawatauza wala kutumia dawa za kuleva, hawatajichukulia sheria mikononi, hawataiba wala kudhulumu, hawatajilimbikizia mali, hawatatega kazini, watakaa mbali na uasherati na maovu mengine yote. Taifa la wacha Mungu lina amani , upendo, umoja na mshikamano. Hivyo lina nafasi kubwa ya kusonga mbele. Lakini ni kazi ngumu sana kuongoza Taifa la watu waliotekwa na ibilisi.
Natoa changamoto kwa viongozi wa dini zote nchini, kuhakikisha mnawajengea waumini wenu, misingi ya madili mema. Waumini wenu wakifuata mafundisho ya Mungu, Taifa litakuwa na raia wema, wachapakazi, maovu ndani ya jamii yatapungua sana kama si kumalizika kabisa.
Vilevile nitumie nafasi hii, kuwakumbusha waumini wa dini zote nchini, kuendelea kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana. Ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuheshimu dini ya mwenzake. Hakuna dini bora kuliko nyingine, dini zote ni sawa, tofauti yake, ni taratibu za namna ya kuabudu. Tofauti hizi haziondoi haki yetu ya kuwa watoto wa Baba mmoja Mungu, walio katika nyumba moja ambayo ni Tanzania. Pendaneni, kwani maandiko matakatifu, yanatufundisha kuwapenda hata maadui wanaotuudhi.
Kitabu cha Mathayo, mlango wa 5, mstari wa 43 hadi 45 unasema hivi, nanukuu; “Mmesikia kwamba imenenwa umpende jirani yako, na umchukie adui yako, lakini mimi nawaambia, wapendeni adui zenu , waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni, maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema , huwanyeshea mvua wenye haki na wasio na haki.”
Baba Askofu Mkuu;
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Nitumie nafasi hii kukupongeza Baba Askofu Alen Siso, kwa namna Mungu alivyokuinua, hatimaye leo umesimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Teule la Mashariki na Pwani. Naamini kuchaguliwa kwako, hakukuja kwa bahati bali “BWANA AMEKUCHAGUA, NA ANA HAJA NAWE.”
Baba Askofu Siso, tukio hili kwako, ni ile sauti iliyoandikwa katika Kitabu cha nabii Isaya mlango 6 mstari wa 8, ikisema kwamba, nanukuu; “ Kisha nikasikia sauti ya Bwana akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yenu? Ndipo niliposema. Mimi hapa, nitume mimi.”
Ujumbe huu umeelezwa pia katika Injili ya Luka , mlango wa 12, mstari wa 42 hadi wa 43, nanukuu; Bwana akasema, ni nani basi aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye Bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake?”
Baba Askofu Siso, mistari niliyoisoma hapo juu ni ushahidi kwamba umepokea utumishi huu kwa Kuitwa na Kuitika. Sisi sote tuliokusanyika hapa leo, ni mashahidi. Ifanye kazi ya Mungu kwa moyo mmoja. Naamini utakuwa mchungaji mwema, utakaowachunga kondoo wa Mungu, na kuwarudisha zizini wale waliopotea.
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Niwaombe viongozi wote wa kanisa hili, kuanzia wewe Baba Askofu Mkuu, Dkt. Byamungu, kuzidisha mshikamano miongoni mwenu, na kumsaidia Askofu wetu mpya, kufanya kazi hii takatifu kwa ufanisi. Zingatieni maneno ya Mungu kutoka Waraka wa Kwanza wa Petro Mtume, mlango wa 5, mstari wa 2 hadi wa 4, nanukuu ; “Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa bali kwa hiyari, kama Mungu atakavyo,si kwa kutaka fedha ya aibu bali kwa moyo, wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.”
Baba Askofu Mkuu Byamungu;
Askofu Siso;
Ndugu Waumini;
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kuwahakikishia kuwa, nimepokea changamoto zenu mbalimbali mlizosoma kwenye risala yenu. Nimesikia matatizo yenu ya maeneo ya kujenga miradi. Serikali kupitia mamlaka zake, itafuatilia kwa karibu masuala hayo, kuangalia namna bora ya kuyapatia ufumbuzi.
Baada ya kusema hayo, kwa mara nyingine, napenda kukushukuruni kwa kunialika mahali hapa siku ya leo. Nazidi kuwasihi sana watu wa Mungu, msichoke kuliombea Taifa letu, kwani kuna nguvu kubwa ndani ya maombi. Kemeeni njama zote zenye nia mbaya ya kuvuruga Amani, Umoja na Mshikamano wetu. Daima, pendeni kusikiliza mema, msivutike kusikiliza maovu . Nawaachia ujumbe kutoka Kitabu cha Mithali, mlango wa 11, mstari wa 31 hadi 32, unasema hivi; “ Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima, bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali. Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa, bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.”
Mungu awabariki sana. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.