RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameunda Tume ya Uchunguzi (Commission Inquiry) Kuhusu Vitendo vilivyotokana na Uendeshaji wa Operesheni Tokomeza. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jioni ya Ijumaa, Mei 2, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Rais ameunda Tume hiyo kwa mujibu wa kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Kutokana na hatua yake ya kuunda Tume hiyo, Rais Kikwete amemteua Mheshimiwa Jaji na Balozi Mstaafu Hamisi Amiri Msumi kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo. Aidha, Rais Kikwete amewateua Jaji Mstaafu Stephen Ernest Mtashiwa Ihema na Jaji Mstaafu Vincent Kitubio Damian Lyimo kuwa Makamishna. Rais pia amemteua Frederick Manyanda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa Katibu wa Tume hiyo.
Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa uteuzi huu ulianza jana, Alhamisi, Mei Mosi 2014. Taarifa ya Balozi Sefue iliyataja majukumu ya Tume hiyo yatakuwa yafuatayo:
• Kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa.
• Kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza.
• Kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea wakati wa Operesheni Tokomeza.
• Kuchunguza na kubaini kama wapo watu wowote waliokiuka Sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao zilikuwa stahiki.
• Kupendekeza hatua zozote zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka Sheria, Taratibu na Hadidu za Rejea za Operesheni Tokomeza.
• Kupendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro. Uteuzi huo wa Tume hiyo unatekeleza ahadi ya Rais Kikwete ambayo aliitoa wakati anahutubia Bunge Novemba 18, mwaka jana, 2013 mjini Dodoma.
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,