MKE wa Rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid wanatarajiwa kuwa wageni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani, yatakayoadhimishwa na Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kuanzia Mei 4 hadi 5, 2014 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TAMA, Dk. Sebalda Leshabari kwa vyombo vya habari, imesema maadhimisho hayo yataanza Mei 4, 2014 kwa kufanyika Kongamano la kisayansi kwa siku moja litakalofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimhili Jengo la ‘New OPD’ Chumba
no 60.
Dk. Leshabari alisema kilele cha maadhimisho ya siku ya wakunga kitafanyika kwenye uwanja wa Mnazi Mmoja Mei 5, 2014 ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Mke wa Rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete. Alisema siku hiyo washiriki wa maadhimisho hayo watafanyika mandamano kutoka makao makuu ya Wizara ya Afya hadi Viwanja vya Mnazimmoja sehemu ambayo sherehe za maadhimisho zitafanyika.
Alisema mbali na shughuli hizo, kuanzia Mei 4, TAMA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watatoa huduma za afya ya uzazi na mtoto bure katika viwanja vya Mnazimmoja kwa akina mama, watoto, vijana na wanaume kwa siku mbili, mfululizo yaani Mei 4 na 5, 2014.
“…Huduma zitakazotolewa ni Uzazi wa mpango, Chanjo kwa watoto Ushauri na upimaji wa hiari wa virus vya UKIMWI, Uchunguzi wa saratani ya matiti na kizazi kwa akina mama, Utoaji wa hiari wa damu, Elimu na ushauri kuhusu hudma ya Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Wanaume kupata sindano ya Pepopunda (tetanus)…,” alisema Dk. Sebalda.
“…Kauli Mbiu ya Mwaka huu (2014) ni “Wakunga Wataalam Wanahitajika Duniani kwa wingi sasa kuliko siku zote.” (The World Needs Midwives Today Than Ever) Hii inalenga katika kuhakikisha kuwa huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto zinatolewa na Wakunga wenye utalaam kwa kufuata miongozo na viwango vilivyowekwa ili kuchangia katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia namba 3,4, 5 na 6.”
Aidha aliongeza kuwa Tanzania ni mmojawapo ya nchi zenye uhaba wa watoa huduma wenye ujuzi hususani Wakunga katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya ambako ndiko wakinana mama wengi wanapata huduma wakiwa wajawazito, ya kujifungua na baada ya kujifungua.
Siku ya Wakunga Duniani huadhimishwa duniani kote tarehe tano mwezi wa tano ya kila mwaka. Madhumuni ya Maadhimisho hayo ni kuhamasisha Wadau mbalimbali pamoja na Jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa wakunga na shughuli wanazozifanya katika kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi pamoja
na vifo vya watoto wachanga na wenye umri chini ya miaka mitano.