Wafanyakazi Walia na Kodi Mei Mosi, Serikali Yaahidi Kupandisha Mishahara…!

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wakipita kwa maandamano mbele ya mgeni rasmi, Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Mai Mosi jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wakipita kwa maandamano mbele ya mgeni rasmi, Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya Mai Mosi jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki akizungumza katika maadhimisho hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki akizungumza katika maadhimisho hayo.

Mmoja wa viongozi kutoka  chama cha waajili Tanzania.

Mmoja wa viongozi kutoka chama cha waajili Tanzania.

Mmoja wa viongozi kutoka  chama cha waajili Tanzania.

Mmoja wa viongozi kutoka chama cha waajili Tanzania.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wafanyakazi kwenye sherehe za MEI MOSI Dar.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wafanyakazi kwenye sherehe za MEI MOSI Dar.

Na Joachim Mushi, Dar es Salaam

WAKATI Serikali ikiahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) limeitaka Serikali kuonesha dhamira ya kweli ya kupunguza viwango vya kodi kwa wafanyakazi kwani hali hiyo inazidisha makali ya maisha kwa wafanyakazi. Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Nicolas Mgaya alipokuwa akiwahutubia wafanyakazi katika maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema mzigo wa kodi ni mkubwa kwa wafanyakazi wa kada zote hivyo kuathiri mishahara ya wafanyakazi hao. “…TUCTA inaishauri Serikali iwe na dhamira ya kweli ya kuitatua kero ya kodi kwa bajeti ya mwaka 2014/2015…,” alisema katika hotuba yake Mgaya.

Aliishauri serikali kufuatilia maombi yaliyotolewa na TUCTA ya kupendekeza maboresho anuai katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuondoa kero kwa wafanyakazi, ikiwemo mifuko kuainisha mfumo wa ukokotoaji mafao na hatimaye uendane na hali halisi ya maisha ya sasa pamoja na mifuko kuruhusu mwanachama kuwa na uwezo wa kuhama kutoka mfuko mmoja kwenda mwingine bila ya kuathiri mafao yake.

Aidha aliitaka serikali kuangalia suala zima la kuendesha vikao vya majadiliano kati yake na Serikali kwani kuna muonekano ya baadhi ya viongozi kuvipuuza na kusababisha visifanyike kwa visingizio kuwa hakuna fedha za kuendeshea vikao hivyo.

Katibu huyo wa wafanyakazi ameiomba Serikali kulipa deni la wafanyakazi linalotokana na malimbikizo ya fedha za mishahara, likizo, kupandishwa vyeo kwa wafanyakazi na stahili mbalimbali na kuhakikisha hali hiyo haiendelei ili kupunguza migogoro kati ya wafanyakazi na waajiri.

Akizungumzia mchakato wa katiba mpya, Mgaya alisema TUCTA inakerwa na kitendo cha baadhi ya wajumbe wa bunge la Katiba kutumia lugha za matusi, kashfa, kejeli na vurugu zinazofanywa na wajumbe hao katika vikao vya majadiliano. Alisema mabishano na kukinzana kwa hoja ni hali ya kawaida katika jambo kubwa linalofanyika kama la uandaaji Katiba ya nchi lakini yasifikie hatua ya kutukanana na kukashfiana kama ilivyotokea hivi karibuni.

Mgaya aliwashauri wajumbe kuacha kutoa lugha ya kuisema vibaya wala kuikashfu tume ya Jaji Joseph Warioba pamoja na wajumbe wake na hatimaye kuhakikisha wanajadili na kufuata maoni ambayo tume hiyo imekusanya kutoka kwa wananchi.

Serikali Kupandisha Mishahara

Serikali imeahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi katika bajeti mpya ya mwaka 2014/2015. Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipokuwa akiwahutubia wafanyakazi katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi zilizofanyika kitaifa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alisema kama ilivyo ada ya Serikali yake ya kuhakikisha inaboresha viwango vya mishahara na mazingira ya wafanyakazi, kuendana na wakati mwaka huu pia imepanga kuongeza mishahara kwa wafanyakazi. Hata hivyo hakutaja asilimia ya nyongeza ya mishahara hiyo licha ya kuwahakikishia wafanyakazi katika sherehe hizo kuwa Serikali itaongeza mishahara.

Aidha alishauri jitihada zifanywe kukabiliana na hali ya mfumuko wa bei kwani ndiyo kikwazo cha kuimeza nyongeza ya mishahara kwa wanyakazi. Alisema kama hazitawekwa jitihada za kuzuia mfumumo wa bei mfanyakazi awezi kunufaika na nyongeza ya mshahara wake kwani itamezwa na mfumuko wa bei.

Sherehe za maadhimisho ya mwaka huu zilianza kwa maandamano kutoka viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Uwanja wa Uhuru ambapo maandamano hayo yalipokewa na Rais Jakaya Kikwete. Vikundi vya wafanyakazi vilipita kwa maandamano mbele ya mgeni rasmi, Rais Kikwete vikiimba nyimbo huku vikiongozwa na bendi ya Jeshi la Polisi.

Kundi la wafanyakazi walimu ambao ndiyo waliokuwa wengi walivutia zaidi kutokana na nyimbo zao, ambapo walisikika wakipaza sauti za kumjulisha rais Kikwete kuwa hadi wanasherehekea Mei Mosi walikuwa hawajalipwa mishahara yao. Walisikika wakiimba; “…Shemeji mshahara bado, Shemeji mshahara bado, Shemeji mshahara bado, Shemeji mshahara bado…,” walisikika wakiimba.

Kwa tafsiri zao shemeji ni Rais Kikwete ambaye mkewe (Mama Salma Kikwete) ni mwalimu hivyo walikuwa wakimjulisha kuwa bado hawajapata mishahara hadi Mei Mosi.