Kocha Mpya wa Taifa Stars, Nooij Akabidhiwa Mikoba

Mart Nooij

Mart Nooij

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza rasmi Mart Nooij kutoka Uholanzi kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya Taifa (Taifa Stars). Rais wa TFF, Jamal Malinzi amemtambulisha kocha huyo leo (Aprili 26 mwaka huu) kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Akiwa amefuatana na Makamu wake Wallace Karia, amesema anafurahi kumtangaza Nooij na ana matarajio kuwa Tanzania itanufaika na uzoefu wake mkubwa wa ukocha, hasa katika bara la Afrika.
 
“Nawaahidi Watanzania kuwa sitomuingilia kocha katika kazi yake. Kama mimi sitomuingilia kocha, basi hakuna mtu yeyote atakayemuingilia. Tumemwajiri yeye kwa vile ni mtaalamu, hivyo hakuna sababu ya kumuingilia,” amesema Rais Malinzi.
 
Naye Nooij ambaye amepewa mkataba wa miaka miwili amesema yeye ni mtu wa maneno mafupi, hawezi kuahidi kitu lakini ana matarajio ya kuifanya Taifa Stars ifanye vizuri katika mashindano mbalimbali. Amesema kabla ya kukubalia kufundisha Taifa Stars alikuwa na klabu ya St. Georges ya Ethiopia, lakini vilevile amewahi kufundisha mpira wa miguu barani Afrika katika nchi za Burkina Faso, Mali na Msumbiji.
 
NGORONGORO HEROES, KENYA UWANJANI DAR
Timu ya vijana ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Kenya zinapambana kesho (Aprili 27 mwaka huu) katika mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Matokeo ya mechi hiyo ya marudiano itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ndiyo yatakayoamua ni timu ipi kati ya hizo itakayocheza raundi inayofuata katika michuano hiyo dhidi ya Nigeria. Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John Simkoko ilitoka suluhu na Kenya katika mechi ya kwanza iliyochezwa Machakos, Kenya wiki tatu zilizopita, na imekuwa kambini jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kujiwinda kwa mechi hiyo.
 
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 na sh. 5,000 ambapo Kenya iliyowasili nchini jana (Aprili 25 mwaka huu) usiku imefanya mazoezi yake ya mwisho leo (Aprili 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa. Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana wakati Kamishna ni Tarig Atta Salih kutoka Sudan.
 
BEACH SOCCER YAZINDULIWA RASMI
Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach Soccer) inazinduliwa rasmi kesho (Aprili 27 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13. Uzinduzi huo utaanza saa 2 asubuhi. Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo mbalimbali vya jijini Dar es Salaam. Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
 
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT). Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.