WAZIRI Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu, Cleopa David Msuya amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya na amemshauri kutokuvunjwa moyo na kile ambacho amekielezea kama “mambo madogo madogo” yanayoendelea ndani ya Bunge Maalum la Katiba.
Aidha, Mzee Msuya amesema kuwa Rais Kikwete hatasahauliwa kwa kipindi chake cha uongozi kutokana na upanuzi mkubwa wa shughuli za maendeleo.
Mzee Msuya ameyasema hayo, Aprili 23, 2014 wakati alipozungumza kuwashukuru na kuwaaga wananchi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro kufuatia hatua yake ya kunga’atuka katika uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, shughuli ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete iliyofanyika ofisi za CCM Wilaya ya Mwanga. Katika hotuba yake ndefu, Msuya ambaye ameshikilia nyadhifa nyingi za uongozi nchini ikiwamo ile ya kuwa Mbunge wa Mwanga kwa miaka 20 mfululizo amemwambia Rais Kikwete:
“Tunakupongeza kwa kuanzisha uandaaji wa Katiba mpya itakayoongoza Taifa letu la Tanzania kwa miaka 100 na zaidi ijayo. Zoezi hili likikamilika kama ulivyoliweka itatuwezesha kusonga mbele na maendeleo ya umma kwa kasi zaidi chini ya utawala bora unaotabirika. Hii ni shughuli kubwa na muhimu sana kwa wananchi wetu, na Mheshimiwa Rais wala usivunjwe moyo na mambo madogo madogo ambayo yanatokea Dodoma,” alisema Mzee Msuya.
Msuya ambaye alishikilia ubunge kwa jumla ya miaka 39, ikiwamo 20 ya Ubunge wa Mwanga na anajulikana kama “Baba wa Mwanga” amemwambia Rais Kikwete: Tunakupongeza kwa maamuzi makubwa na mazito ya msingi uliyoyafanya kuonyesha njia ya maendeleo kwa Taifa letu la Tanzania ikijumuisha Mwanga”.