ALIYAKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameuliza maswali saba ya msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao. Jaji Warioba ambaye tangu awasilishe Rasimu ya Katiba Desemba 30, mwaka jana amegeuka kuwa adui kwa watu wanaotaka muundo wa serikali mbili, aliuliza maswali hayo jana katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa Katiba.
Akizungumza kwa ukali, Jaji Warioba alisema: “Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati walioupendekeza ni wananchi?
“Sheria inasema uwepo wa Muungano na mapendekezo katika rasimu hayasemi Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa wananchi walitakiwa kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha Muungano.”
Katika swali lake la pili, Warioba alisema kwa nini Tanganyika imevaa koti la Muungano? Kwa kuwa katika ukusanyaji wa maoni wananchi walieleza kuwa Serikali ya Muungano ya sasa siyo ya Muungano, ni ya Tanganyika. Katika swali la tatu alisema wajumbe hao wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi ambao waliieleza tume kuwa Katiba imevunjwa na madaraka ya rais yamechukuliwa na sasa kuna marais wawili katika nchi moja.
“Tume inapewa lawama kubwa, wajibuni wananchi hii tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi? Waambieni ilikusanya maoni hayo kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?” alisema Jaji Warioba katika swali lake la nne.
Katika swali lake la tano, Warioba aliwataka wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu kuwa amependekeza muundo wa serikali tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph Butiku) walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo zilipendekeza muundo wa serikali tatu, kitu ambacho alisema si kweli na hawakuwahi kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia, aliwataka wajumbe hao kujibu swali la sita, kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na badala yake wanageuza rasimu hiyo kuwa imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Katika swali lake la saba, aliwataka wajumbe kujibu kwa nini wanaishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa imeingiza maoni yake, wakati ilikusanya maoni hayo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba?
Alisema badala ya kujadili hoja za msingi, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa lugha za kejeli na matusi kwa baadhi ya watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho alisema si sahihi na kinaweza kuligawa taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi.
Katika uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Dk Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole.
Amshukia Lukuvi
Katika maelezo yake, Jaji Warioba alieleza kushangazwa kwake na wajumbe kulitumia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama mfano wa kuwashawishi Watanzania kukubaliana na matakwa yao ya kutaka kupinga mfumo wa serikali tatu.
“Nchi hii imekuwa na matatizo ya rushwa na ufisadi, lakini hakuna hata siku moja mtu amesema jeshi linaweza kushika madaraka. Leo kwa sababu ya madaraka mnaingiza jeshi na mchakato wa Katiba katika makundi.”
Licha ya kutomtaja mlengwa, kauli hiyo ilionekana kumlenga Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi ambaye Aprili 13, mwaka huu aliwataka wananchi kupinga muundo wa serikali tatu, akisema la sivyo jeshi linaweza kuchukua madaraka. Akiwa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi alisema muundo huo ukipita, nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.
Kauli kama hiyo pia iliwahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
“Msiliingize jeshi katika siasa za makundi na inakuwa mbaya zaidi kama mkienda katika makanisa na kutoa kauli za namna hii,” alisema Warioba na kuongeza:
“Umoja wetu, amani na utulivu kwa kiwango kikubwa mhimili wake ni viongozi wa dini. Wamekuwa wakihubiri umoja, amani na mshikamano, hivyo tusiingize siasa za makundi kwenye makanisa na misikiti.”
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge hilo kukumbuka wajibu wao wa kuwaunganisha wananchi na kuwataka waachane na kauli za kejeli, kuudhi na matusi kwani zinaweza kuleta mgawanyiko na mpasuko nchini.
“Nimekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu lakini sijawahi kuona taasisi yenye uzalendo wa hali ya juu kama JWTZ,” alisema Warioba.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, kuanzia mwaka 1985 hadi 1990, alisema: “Katika ziara zangu mikoani nilikuwa nikikutana na wanajeshi na kunieleza matatizo yao. Licha ya wakati huo serikali za mataifa mengine zilikuwa zikipinduliwa na jeshi, hapa kwetu ilikuwa tofauti, walikuwa na uzalendo wa hali ya juu licha ya kuwa hali yetu kiuchumi ilikuwa mbaya,” alisema.
Alisema wakati huo wanajeshi walikuwa wakivaa sare zilizochakaa na viatu vilivyopasuka, lakini hawakufikiria kuipindua Serikali.
Alisema hata katika vita dhidi ya Uganda, wanajeshi wa Tanzania walishinda kwa sababu ya uzalendo na siyo vifaa vya kisasa vya kivita… “Inashangaza kuona watu wanatolea mfano mmoja tu wa kama wanajeshi wasipolipwa; kwa nini wasiseme mawaziri au watumishi wa serikali wasipolipwa?”
Alisema kauli hiyo ni sawa na kuwaeleza wananchi kuwa jeshi ni baya na kama ikipita Katiba isiyoendana na matakwa ya walio wengi jeshi litachukua nchi. Alisema wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikikusanya maoni ya wananchi, wanajeshi na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini walijikita zaidi kutoa maoni ya kuimarishwa kwa ulinzi na usalama na siyo mambo mengine.
“Tatizo ambalo walitueleza ni kuchoshwa na kitendo cha kupiga mizinga 21 kwa Amri Jeshi Mkuu wakiwa Dar es Salaam na wakiwa Zanzibar. Walisema kwa nidhamu ya jeshi, Amri Jeshi Mkuu ni mmoja tu. Nadhani mngewaondolea kero hiyo na si mambo mengine,” alisisitiza.
Kigwangalla
Kwa upande wake, Dk Kigwangalla alisema kama tatizo ni Muungano ni vyema suala hilo likarejeshwa upya kwa wananchi ili watoe maoni yao kwa sababu mchakato huo sasa umehamia katika muundo wa Muungano pekee.
“Mchakato huu si wa kuifufua Tanganyika na kuvunja mkataba wa Muungano na siyo wa kubadili muundo wa utawala. Mambo haya yalihitaji mchakato unaojitegemea,” alisema.
Alisema tume zote zilizotoa mapendekezo ya Serikali tatu zilikuwa na asilimia ndogo ya watu waliounga mkono kama ilivyo kwa Tume ya Jaji Warioba.
CHANZO; Mwananchi