WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia leo amemwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda katika mazishi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Marehemu Moshi Chang’a.
Katika mazishi hayo wamehudhuriwa mamia ya wakazi wa Manispaa ya Iringa na viongozi wa serikali kutoka mikoa mikoa mbali mbali nchini pia spika wa bunge Anne Makinda alitumia nafasi hiyo kuueleza umma siri nzito iliyofichika dhidi yake ya marehemu Chang’a mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi kuwa bila marehemu huyo asingeweza kuwa mbunge kutokana na kubanwa na chama cha upinzani cha NCCR Mageuzi kwa kipindi hicho.
“Mimi nimekuwa kwa niaba yangu mwenyewe na Jimbo la Njombe Kusini ambalo mimi ni mbunge wake…mwaka 1995 marehemu alikuwa ni katibu wa CCM Njombe na ndio mwaka ambao mfumo wa vyama vingi ulianza na yeye ndie alikuwa katibu na jimbo hilo upinzani ulilizingira kweli na hata kwa kukanyanga mguu kulikuwa hakuna ila bila Chang’a kweli jimbo hilo niseme ukweli lingekuwa limechukuliwa na Upinzani na kwa kipindi hicho chama chenye nguvu zaidi kilikuwa ni NCCR Mageuzi,”
Akizungumza wakati wa kutoa salama mbalimbali kwa viongozi mjini Iringa Spika Makinda alisema kuwa kwa mara ya kwanza mwaka 1995 alibanwa kupita kiasi na NCCR Mageuzi katika jimbo lake la uchaguzi la Njombe kusini na kuwa bila marehemu huyo ambae kwa kipindi hicho alikuwa ni katibu wa CCM wilaya ya Njombe kamwe asingeweza kuwa mbunge.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa injinia, Stella Manyanya alisema kuwa mkoa wake amempoteza kiongozi mzalendo na aliyependa kazi yake na kuwa hata akiwa safarini hakuwa na shaka na utendaji kazi wa mkuu huyo wa wilaya na kuwa siku zote mbali ya kuongoza kama kiongozi wa serikali ila wakati mwingi alitumia kuwahubiria upendo wananchi wa wilaya yake. Kwani alisema kuwa alikuwa hawezi kuanza mkutano bila kumhubiri mwenyezi Mungu mbali ya kuwa yeye alikuwa muumini wa dini ya Kiislam ila alikuwa akihubiria dini ya kikristo.
Hata hivyo alisema kuwa hadi kesho anaamini alishinda ubunge jimbo hilo mwaka 1995 si kwa uwezo wake bali alishinda kwa uwezo wa marehemu Chang’a ambao alionyesha uwezo mkubwa wa kumnadi na hata kufanikiwa kuwa mbunge wa jimbo hilo na leo kuwa Spika wa Bunge. Alisema iwapo angekwama kuwa mbunge mwaka 1995 basi yawezekana leo asingekuwa spika kwani angekuwa amekata tamaa ama angekuwa mbunge mwingine katika jimbo hilo.
Aidha alisema mbali ya kushinda ubunge wake bado wapinzani walikwenda mahakamani kupinga matokea ila Chang’a alisimama na makada wenzake wawili moja akiwa ni marehemu sasa katika kumtetea mahakamani kwa miaka minne yote na mbali ya hujuma kubwa zilizokuwa zikifanywa na Halmashauri ya Njombe kwa kuharibu baadhi ya nyaraka za ushahidi ili kuwawezesha NCCR Mageuzi kushinda kesi hiyo japo kwa Chang’a walishindwa kutokana na kuwa na nyaraka hizo kwa mwenendo mzima wa mchakato wa uchaguzi huo hadi mahakama ilipompatia ushindi yeye kama mbunge halali wa jimbo hilo.
“Leo nafanya kazi hii ya uspika kwa kuwa Chang’a ndie aliyeniweka hapa na bila yeye kujituma mimi nisingesimama hapa kama spika…jamani nasema tuendelee kujituma katika kazi zetu kama alivyofanya marehemu Chang’a nasema kila mmoja atapimwa utendaji kazi wake hapa duniani ”
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mbeya Abas Kandoro akimuelezea Chang’a wakati wa kutoa salam hizo alisema kuwa kamwe hata sahau utendaji kazi wa mkuu huyo wa wilaya ambae amepata kufanya nae kazi katika wilaya ya Makete ambapo yeye akiwa mkurugenzi Chang’a alikuwa ni kiongozi wa CCM wilaya hiyo na baada ya kwenda Mbeya pia Chang’a amefanya kazi kama mkuu wa wilaya katika mkoa huo.
Kandoro alisema kuwa utendaji kazi na utumishi uliotukuka wa Chang’a ni mfano wa kuigwa kwa watumishi wengine wa umma katika Taifa hili.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Christine Ishengoma alisema kuwa mkoa wa Iringa umepata pigo kubwa kwa kifo cha mkuu huyo wa wilaya hasa ukizingatia mchango mkubwa wa kimaendeleo ambao amepata kuonyesha ndani ya mkoa na nje ya mkoa na kuwa kamwe mkoa utaenzi yote aliyoyaacha.
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema wananchi wa Manispaa ya Iringa na Mkoa wa Iringa tumeendelea kupoteza wakuu wa wilaya na Chang’a pia tumepata kumpoteza Mkuu wa wilaya ya Tabora na kuwa viongozi hao wote ni pengo kubwa kwa Taifa.
Mbunge Msigwa alisema kuwa akiwa kama mbunge wa jimbo hilo na kiongozi wa Chadema wilaya hiyo amepokea kwa masikitiko kifo hicho na kama viongozi wanapaswa kuangalia ni barua gani ambayo inaachwa kwa jamii baada ya kuondoka na kuwa Chang’a alikuwa ni kiongozi asiyependa kumchukia mtu na kila wakati alikuwa ni mtu wa kucheka na kila mmoja.
Awali akiwasilisha salama za serikali waziri Ghasia alisema kuwa kifo hicho kimeacha pengo kubwa na kumtaja marehemu Chang’a katika mkuu wa wilaya wa mfano ambae hakupenda kukataa wala kuonyesha kupinga kwa sehemu yeyote anayopangiwa kwenda kuwakilisha wananchi.
Viongozi wengine waliopata kushiriki mazishi hayo ni pamoja na Msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete katika masuala ya siasa Ikulu, Rajab Luhwavi na viongozi kutoka mkoa wa Mwanza, Singida, wabunge wa Tanzania akiwemo mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati na Lediana Mafulu (CCM), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba kutoka Mkoa wa Iringa na wakuu wa wilaya mbali mbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamwoto, Mkuu wa wilaya ya Iringa, Dk. Letisia Warioba, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita na wengine wengi.