Dodoma,
HABARI zilizotufikia muda huu kutoka bungeni mjini Dodoma ni kwamba; Mbunge wa Ilemela kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekiel Wenje ametolewa nje ya Bunge katika kikao kinachoendelea hivi sasa mjini Dodoma.
Wenje ametolewa nje ya bunge na Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba ambaye ndiye anayeongoza kikao hicho, baada ya kuvuana huku akihoji kuwa mwenyekiti huyo anaongoza kwa kuwaburuza wabunge.
Wakati Wenje akiwasha kipaza sauti kuzungumza tayari kulikuwa na mabishano yakiendelea kati ya Mbunge Moses Machali (NCCR-Magezi Kasulu Mjini) aliyekuwa akihoji muda mfupi aliokuwa amepewa mbunge wa CHADEMA, Tindu Lisu kuthibitisha kauli yake ambayo alidai mmoja wa mawaziri wenye dhamana na kodi amelidanganya bunge katika majibu yake.
Hata hivyo kwa mujibu wa maelezo ya Wenje baada ya kutolewa nje anasema mbali na mabishano hayo alitaka kutoa taarifa ya uwepo wa taarifa za kuingia kwa samaki wa sumu nchini jambo ambalo ni hatari kwa wananchi.
Kitendo cha kutolewa kwa Mbunge Wenje bungeni hakikuwapendeza wabunge wa CHADEMA hivyo nao kutoka nje ya Bunge na hivi sasa bado wanazungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi huku bunge likiendelea bila ya wao kuwepo.
Tutawaletea habari zaidi kadri zitakavyotufikia kutoka mjini Dodoma.