Jalada la Chenge utata mtupu


Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge

HATIMA ya jalada la uchunguzi dhidi ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, bado ni kizungumkuti, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Elieza Feleshi, kusisitiza jana kuwa mpaka sasa halijafika ofisini kwake.
Lakini alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, alisema: “Kama hajalipata, atalipata soon (hivi karibuni).”

Wiki iliyopita Dk Hoseah akiwa mkoani Arusha alitangaza mbele ya waandishi wa habari kuwa uchunguzi wa fedha alizoweka Chenge nje ya nchi umekamilika na jalada lake kwenda kwa DPP, lakini kesho yake DPP Feleshi alisema halijafika kwake.

Hata hivyo,uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa jana kwenye ofisi ya DPP ulibaini kuwa jalada hilo halijafika.
Feleshi alisisitiza kuwa mpaka sasa jarai hilo halijafika ofisini kwake. “Mpaka sasa halijafika kwangu, labda muulizeni Hoseah kwamba alilileta lini,” alisisitiza Feleshi.

Dk Hoseah alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema: “Mambo ya majalada si ya kuandika kwenye magazeti, bali ni mambo ya kiutendaji kati ya ofisi yake na Mkurugenzi wa Mashitaka”.

Dk Hoseah alisisitiza: “Kama hajalipata atalipata soon (hivi karibuni). Ninachojua ni kwamba tayari tumewasilisha jalada hilo kwenye ofisi ya DPP, lakini bado mnaendelea kuuliza mambo hayo, suala la majalada ni ya mimi na DPP.” “Kwa nini mnapenda kufuatilia mambo yasiyowahusu. Tangu lini mambo ya majalada yakaandikwa kwenye magazeti, ni ushabiki au kuna malengo ya kutugombanisha? Sioni kama ni habari hii na siwezi kuingia kwenye mjadala huo.

“Kama suala hilo mnafuatilia hivyo , mnapaswa kuja kwenye masjala ya Takukuru ili waweze kuangalia majalada yaliyopo si la Change peke yake. ”Kwa mujibu wa Dk Hoseah, hakuna mantiki ya kukaa na kuhoji kuhusu jalada la Chenge, kwa sababu wao ndio watendaji wakuu na watu wengine hawapaswi kulifuatilia suala hilo mpaka watakaposikia zimechukuliwa hatua nyingine za kisheria.

Kwa upande wake DPP, Feleshi alisema hadi muda huo wa mchana jana, jalada hilo lilikuwa halijafika ofisini kwake hivyo hawezi kusema chochote tena bila kuliona kwanza.

“Kuna majalada mengi yametoka Takukuru, mengine yamekuja kwa ‘Dispach’na mengine yamekuja kwa njia ya kawaida, lakini la Chenge bado halijafika, ofisi ya maslaja ndio hii unaweza kuangalia mwenyewe ili uweze kuhakiki,” alitoa ruksa DPP Felesh.

Mvutano wa Hoseah, DPP
Baada ya Hosea kusema jalada la Chenge liko kwa DPP wiki iliyopita, Feleshi alipoulizwa na gazeti hili alisema: “Niko safarini subiri hadi wiki ijayo…, kwanza ashtakiwe kwa kosa gani..…acheni siasa nyie.”

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kama jalada hilo limefika mezani kwake alimtupia mzigo Dk Hoseah na kumtaka aseme ni siku gani alipeleka jalada hilo kwake akisema: “Huyo Hoseah ameseme ni tarehe gani alileta jalada hilo kwangu?”

Lakini, Dk Hoseah alipoulizwa na Mwananchi baada ya maelezo hayo ya DPP, alihojiakisema: “Kwani kila kitu kinachopelekwa kwake (DPP) lazima akione je, ameangalia kwenye legistry (masijala)?”

“Mimi nimeongea na ninyi juu ya suala hilo vya kutosha, hivyo muulize zaidi DPP,”

Dk Hoseah alisema mjini Arusha wiki iliyopita kuwa taasisi yake imekamilisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Chenge na kwamba jalada limepelekwa kwa DPP kwa hatua zaidi.

Alifafanua kwamba,Chenge atashtakiwa chini ya kifungu cha 27 cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007.Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu akiwa na mali ambazo hazilingani na kipato chake alichokipata akiwa madarakani, au baada ya kuondoka ni kosa kisheria.

Chenge alikutwa na kiasi hicho cha fedha zenye utata mwaka 2008 baada ya uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO), lakini ikabainika fedha hizo hazikuwa na uhusiano na biashara hiyo.

Fedha hizo alizoziita vijisenti ndizo zilizopelekea Chenge kung’atuka katika wadhifa wa Uwaziri wa Miundombinu mwaka 2008.
CHANZO; Mwananchi.