Kambi ya UN Yashambuliwa Sudan Kusini, Watu Wauwawa

Kambi ya UN Yashambuliwa Sudan Kusini, Watu Wauwawa.

WATU wenye silaha wamewaua raia kadhaa waliokuwa wamehifadhiwa katika kituo cha Umoja wa Mataifa mjini Bor katika Jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini, katika mauaji yaliyoelezwa na waziri kuwa ni ya kulipa kisasi. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power, alisema watu wasiopungua 20 waliuawa jana, baada ya raia waliojihami kwa silaha kuvamia kituo hicho cha Umoja wa Mataifa na kuanza kuwafyetulia risasi raia wenzao kutoka kabila hasimu.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS, ulisema watu hao waliingia katika kituo hicho kama waandamanaji wa amani, wakiomba kuwasilisha waraka, lakini walivyoingia wakaanza kuwafyetulia risasi wakimbizi. Vikosi vya UNMISS vilijibu mashambulizi kwanza kwa kufyatua risasi hewani na baadaye mapigano makali yaliibuka kabla ya wapiganaji hao kukimbia.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephanie Dujarric alilaani shambulio hilo dhidi ya raia na kusema linachochea zaidi mgogoro wa kikabila, ambao umelichagiza taifa hilo changa kabisaa kwa zaidi ya miezi minne sasa.

“Shambulio hilo dhidi ya eneo ambako raia wanalindwa na Umoja wa Mataifa ni uchochezi mkubwa, katibu mkuu anazikumbusha pande zote kwamba shambulio lolote dhidi ya walinda amani halikubaliki, na ni sawa na uhalifu wa kivita.

Katibu Mkuu anatoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini kuchukua hatua zote kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, ulinzi wa maeneo ya raia nchini Sudan Kusini, na pia anatoa wito kwa pande zote kujizuwia na vitendo au matamshi ambayo yanaweza kuchochea hali zaidi,” alisema Dujarric.

Maelfu wameuawa na zaidi ya watu milioni moja wameyakimbia makaazi yao tangu mapigano yaibuke mwezi Desemba kati ya wafuasi wa makamu wa rais alieondolewa Riek Machar na vikosi vitiifu kwa rais Salva Kiir. Vikosi hivyo pinzani vinatokea katika makabila hasimu, na hivyo kuongeza hatari ya ukabila katika mgogoro huo.

Watu wanaokadiriwa kufikia alfu 65 wametafuta hifadhi katika vituo vya Umoja wa Mataifa kama kile kilichopo mjini Bor. Raia wapatao alfu 5 waliokuwepo kambini hapo wakati mashambulizi yalipofanyika wanasemekana kutoka katika kabila la Riek Machar, ambaye inadaiwa kuwa jaribio lake la kumpindua rais baada ya kuondolewa katika nafasi yake lilisababisha machafuko hayo.

Balozi Power alisema Marekani itashirikiana na washirika wake kubaini wahusika wa shambulio hilo la kinyama na kuwafikisha mbele ya sheria. Alizitolea wito pia nchi zilizojifunga kuchangia wanajeshi zaidi katika kikosi cha UNMISS kuharakisha kuwapeleka.

“Watu wa Sudan Kusini wanastahili kuwa na fursa ya kuanza kuijenga upya nchi yao na kuziendeleza taasisi za kitaifa na kimajimbo, ambazo wanazihitaji kuirudisha nchi hiyo katika njia ya utulivu na demokrasia,” alisema balozi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Waziri wa mawasiliano wa Sudan Kusini Michael Makuei alisema idadi kubwa ya wanamgambo walikwenda kulipiza kisasi kwa hatua ya waasi kuuteka mji wa mafuta wa Bentiu siku mbili zilizopita, wakitumai kuwauwa raia waliozingirwa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Waziri Makuei alisisitiza kuwa visima vya mafuta vilikuwa mikononi mwa serikali, lakini uchimbaji ulisimama mjini Bentiu, ukanda muhimu wa mafuta, kwa sababu miundombinu iliharibiwa katika mapigano. Bor ni moja ya miji iliyoshudia mapigano makali sana, ikibadilishwa udhibiti kati ya waasi na vikosi vya serikali mara kadhaa.

Mapigano ya hivi karibuni yanakumbushia shambulio lingine lilifanywa mwezi Desemba na watu wenye silaha dhidi ya kituo cha Umoja wa Mataifa katika mji wa Akobo, uliko pia jimbo Jonglei, ambapo raia 11 waliuawa na askari wawili wa Umoja wa Mataifa kutoka nchini India.

-DW