Dodoma
MBUNGE wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), amewalipua watendaji wa umma kwa kueleza kuwa ndiyo maadui wakubwa wa Serikali na siyo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Amesema mipango yao isiyotekelezeka ndiyo inasababisha wananchi wakose imani na Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lusinde alitoa kauli hiyo bungeni, wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 iliyowasilishwa juzi na waziri wa wizara hiyo, Prof. Jumanne Maghembe.
Mbunge huyo akiendelea kuchangia, alisema wataalamu wa serikali hawana msaada wowote hivyo akataka wasijumuishwe kwenye misafara ya Rais pindi anapotembelea nje ya nchi.
“Juzi hapa tumemuona, Rais Jakaya Kikwete akiwa nchini Malasia, lakini nimeshangazwa na hatua ya rais kuomba ‘business card’ za wataalamu nchini humo bila watalaam wetu nao kufanya juhudi za dhati kujifunza teknolojia yao.
…Rais baada ya kuvutiwa na utaalamu wa watu wa Malasia anaamua kuchukua mawasiliano akisema nitakutafuta sasa. Sasa hawa huwa wanaenda kufanya nini kama hamjifunzi kutoka kwa wenzetu hao, basi msiwe msiende kwenye msafara wa rais kwasababu hamna faida yoyote,” alisema Lusinde.
Kuhusu sekta ya kilimo, Lusinde alisema Serikali bado haijafanya juhudi za makusudi za kukifanya kiweze kupiga hatua na hivyo kuwa mkombozi kwa wakulima. Na kuongeza kuwa sekta hiyo inahitaji pembejeo za kisasa.
Mbunge huyo alisema anashangazwa na kitendo cha kilimo kutopewa kipaumbele na vyombo vya maamuzi.
“Sekta ya kilimo ndiyo inatakiwa kupigiwa kelele na si umeme kama mnavyofanya hapa waheshimiwa wabunge. Kama mnafikiri kilimo ni mchezo basi tuanzishe Shamba la Bunge tuone kama wote hamjakimbia.
…Sekta ya kilimo hamkipi kipaumbele na badala yake mnakomaa na umeme tu au kwa vile mnaogopa nyama zenu zitaoza, kilimo ndiyo sekta ya msingi inayopaswa kupigiwa kelele ili serikali ikiboreshe,” alisema Lusinde.
Hivyo akaitaka Serikali kuhakikisha inapeleka mbolea kwa wakulima kama inavyofanya kwenye Uchaguzi Mkuu na si kuendelea kupiga porojo kwamba inaboresha sekta ya kilimo ili hali si hivyo.
“Serikali ni ya ajabu sana, wakati wa uchaguzi masanduku ya kupigia kura yanafika kila kijiji, lakini linapokuja suala la kupeleka mbolea kwa wakulima haifanyi hivyo, sasa hapa ndiyo kweli tunaboresha kilimo kweli. Sasa hii hali isipobadirishwa huko mbele ni bora tusipitishe bejeti zote ili turudi kwenye uchaguzi, potelea mbali maana tumechoka na porojo badala ya vitendo, wengi wetu tumekula mlo mmoja mpaka leo tupo hapa.
Mbunge huyo akiendelea kuzungumza aliitaka serikali kuboresha kilimo cha zabibu mkoani Dodoma kwa kuhakikisha inaundwa Bodi ya Zabibu ili iwe kiunganishi kukuza zao hilo.
“Nataka Waziri aje atuambie ni lini, Bodi ya Zabibu itaundwa ili na sisi wananchi wa Dodoma ambako zao hili linapatikana kwa wingi tuweze kuboresha kilimo hicho.
Haiwezekani mnaunda bodi nyingine tu huku zabibu mkiipa kisogo, mnaona bora kuunda bodi ya tumbaku kuliko zabibu au mnataka watu wafe. Hata Mungu anatushangaa, mvua zikinyesha viongozi wa dini wakusanyika kuomba ili tuondokane na mafuriko na isiponyesha wanaomba ili mvua zinyeshe, hivi sisi ni watu wanamna gani,” alihoji Lusinde.