Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
MVUA Kubwa inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam ambayo imesababisha mafuriko imeua zaidi ya watu nane maeneo mbalimbali yaliyokubwa na mafuriko hayo. Kwa mujibu wa taarifa ambazo dev.kisakuzi.com imezipata kutoka kwa baadhi ya vikosi vya uokoaji watu nane wamebainika kufariki dunia huku kukiwa na tetesi ya idadi hiyo kuongezeka kutokana na taarifa zinazoendelea kukusanywa.
Mmoja wa wajumbe wa kikosi cha uokoaji cha vijana jijini Dar es Salaam, akizungumza na dev.kisakuzi.com kwa masharti ya kutotaja jina kwa kuwa yeye si msemaji wa kikosi hicho, alisema hadi sasa wameshuhudia watu wanane wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliotokea.
“…Tumeshuhudia maiti nane hadi sasa ambazo zimehifadhiwa katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam…Katika Hospitali ya Temeke kuna maiti moja ambayo imetokea Mto Mzinga Mbagala, Hospitali ya Muhimbili kuna maiti nne na Hospitali ya Mwananyamala kuna maiti tatu,” alisema mjumbe huyo kijana.
Kwa upande wake mmoja wa viongozi wa Kikosi cha Msalaba Mwekundu, Kassim Abdalah akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema wapo baadhi ya raia wamepoteza maisha kutokana na mafuriko hayo japokuwa alisema takwimu halisi za vifo hivyo (idadi) kikosi chake hakina.
“…Kwa leo hakuna taarifa yoyote ya kifo ila kwa jana wapo watu walipoteza maisha, lakini hapa sina idadi kamili ya vifo hivyo unaweza kuipata kwa viongozi wetu wa juu…,” alisema Abdalah.
Aidha alisema wapo baadhi ya wananchi waathirika wa mafuriko hayo takribani 230 ambao wamezikimbia nyumba zao kutokana na kukumbwa na maji ya mafuriko na wamejikusana katika kambi nne zilizopo eneo la Jangwani, eneo la Fire, eneo la Nyati na Jengo la Yanga huku wakihitaji misaada.
Alisema Msalaba Mwekundu wamewagawia mablanketi kwa ajili ya kujistili na baridi kutokana na nguo zao nyingi kulowa kwenye mafuriko. “…Kwa sasa tunachokifanya ni kuwagawia blanketi hizi kwa ajili ya kujikinga na baridi maana nguo zao nyingi zimelowa kutokana na mafuriko,” alisema Abdalah.
Kikosi cha mbwa na farasi toka Jeshi la Polisi nacho kinaendelea kutoa msaada wa kusaka miili ya watu zaidi wanaohofiwa kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo. dev.kisakuzi.com imeshuhudia vijana wa skauti wa kikosi cha uokoaji kutoka kwa Watanzania wenye asili ya India kikishirikiana na Jeshi la Polisi wakitafuta miili zaidi pembezoni mwa Mto Msimbazi eneo la Tabata Matumbi.
Mmoja wa viongozi wa Skauti kutoka kikosi hicho, Alilaza Bandal alisema walipata taarifa kutoka kwa baadhi ya watu kuwa kuna maiti imenasa eneo hilo hivyo walifika na kukagua eneo lote wakishirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha Mbwa na Farasi na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji lakini hawakukuta maiti yoyote.