Stamico yatenga mil 140 kuwasaidia wachimbaji wadogo


Banda la STAMICO ndani ya maonesho ya Nishati na Madini Mnazi Mmoja.

Na Ismail Ngayonga na Mpoki Ngoloke-Maelezo

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limepanga kutumia kiasi cha sh milioni 140 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwa wachimbaji wadogo katika mgodi wa Lwamgasa uliopo wilayani Geita Mkoani Shinyanga.

Hayo yamebainishwa leo (jana) na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko wa Stamico, Lola Mwanga katika maonyesho ya Wizara ya Nishati na Madini ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Aliongeza kuwa makusudio ya kuwasaidia wachimbaji hao yametokana na mgodi huo kuwa na wachimbaji wadogo kuwa wengi waliojiunga katika vikundi pamoja na kuwa na leseni ya uchimbaji katika maeneo yao.

Alisema Stamico imekusudia kuwasadia wachimbaji wadogo kuchimba madini kwa kutumia utalaamu wa kisasa zaidi ili uchimbaji wao uwe endelevu na kuongeza ajira pamoja na kuchngia katika pato la taifa.

Alisema kuwa mwezi septemba mwaka 2010 stamico ilifanya utafiti kwa kupeleka timu ya wataalamu katika migodi mbalimbali ya wachimbaji wadogo nchini ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji hao katika shughuli zao za kila siku.

Aliongeza kuwa miongoni mwa migodi iliyofanyiwa utafiti huo na stamico kuwa ni Londoni uliopomkoani Singida, Nyarugusu uliopo Geita mkoani Shinyanga pamoja na mgodi wa Lwamgasa uliopo pia katika mkoa wa Shinyanga.

Akifafanua zaidi Mwanga anasema katika utafiti miongoni mwa changamoto zilizoonekana kuwakabili wachimbaji hao kuwa ni matatizo ya kufulika kwa maji katika machimbo, ukosefu wa vifaa vya kutoa mchanga ndani ya migodi pamoja na ukosefu wa utaalamu wa uchimbaji na uchenjuaji madini.

Kwa mujibu wa Lola, Stamico mwishoni mwa mwaka jana ilipatiwa na Serikali kiasi cha Tsh Milioni 200 ikiwa ni mkopo kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo, na katika kuhakikisha kuwa mkopo huo utaleta tija kwa iliyokusudiwa waliamua kufanya utafiti katika migodi hiyo mitatu.

Alivitaja vifaa vitavyonunuliwa na kampuni kuwa ni pampu za kuvutia matope kutoka migodini, mashine za kusaga mawe, madawa ya kusafishia madini, kifaa cha kusafirishia udongo kutoka machimboni.

“Mwishoni mwa mwaka jana Serikali ilitoa kiasi cha Tsh Bilioni 1 kwa makampuni mbalimbali yanayojishughulisha na uchimbaji wa madini, Stamico ilipewa kiasi cha Tsh Milioni 200 ambapo zitarudishwa kwa njia ya riba” alisema Lola.

Aidha aliongeza kuwa pamoja na mkopo ho ulitolewa na Serikali kuhudumia wachimbaji wadogo, shirika lake pia limefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya mazungumzo ya awali na mwekezaji kutoka nchini Afrika Kusini ili kuongeza nguvu za pamoja za kuwasaidia wachimbaji hao.