Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
Serikali imetoa wito kwa waandishi wa habari kuzingatia weledi taaluma ya habari wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka kuandika habari zinazotoa hukumu juu ya masuala mbalimbali yanayotokea katika jamii na zinazolenga kuwashawishi wananchi kufanya mambo yasiyokuwa na maslahi kwa taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Bw. Assah Mwambene alipozitembelea ofisi za magazeti ya The Guardian Ltd na Nipashe yanayochapishwa na kampuni ya IPP Media kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na watendaji wa magazeti hayo ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Akizungumza na watendaji wa magazeti hiyo amesema kuwa taaluma ya habari hapa nchini ndiyo inayotoa mwelekeo wa nchi kutokana na umuhimu ilio nao katika kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbalimbali yanayotokea nchini na kuongeza kuwa kuwepo wa vyombo vya habari nchini kumechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya sekta mbalimbali nchini
.
Amesema kuwa serikali kwa upande wake inatambua mchango mkubwa unaotolewa na magazeti hayo hapa nchini na kuongeza kuwa itaendelea kuheshimu na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.
“Sisi tunajivunia uwepo wenu kutokana na jukumu kubwa mlilonalo kwa watanzania maana bila ninyi hatuna Idara ya Habari, napenda nitumie fursa hii kuipongeza kampuni ya IPP hasa wahariri wa gazeti la The Guardian kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa kutoa kipaumbele kwa ajenda zenye mustakabali mwema wa taifa letu” Amesema.
Ameeleza kuwa heshima ya vyombo vya habari hususan magazeti hapa nchini haitokani na uchapishaji wa habari zenye lengo la kuuza gazeti bali utoaji wa habari zenye kutoa kipaumbele juu ya mambo ya msingi na yenye maslahi kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa taaluma ya habari hapa nchini inapaswa kuheshimiwa na waandishi wa habari wenyewe amabao ndio wadau muhimu wa tasnia hiyo kutokana na mchango mkubwa walio nao katika kuleta mabadiliko katika jamii.
“Taaluma ya habari hapa nchini inapaswa kuheshimiwa, kwa upande wetu kama Idara sasa tunatoa msukumo kwa waandishi wa habari kuwa na sifa na ndio maana tunatoa vitambulisho kwa waandishi wa habari wenye sifa kuhakikisha kuwa wanaofanya kazi ya uandishi wa habari ni wale tu wenye sifa ya kuwa na taaluma ya habari”.
Kuhusu mchakato unaoendelea nchini wa kupata katiba mpya amesema kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuepuka uandishi wa habari zenye ushabiki na uchochezi kutokana na unyeti wa zoezi lenyewe na jinsi linavyogusa maisha ya watu na kusisitiza kuwa vyombo vya habari ndivyo vitakavyoisaidia jamii kujua hali halisi ya mambo yanayotokea katika zoezi hilo.
“Baadhi ya vyombo vimesahau majukumu yake kwa kuanza kuonyesha misimamo kwa kuwaamulia wananchi katika masuala ya msingi hasa kwenye mchakato unaoendelea wa kupata katiba mpya, jambo hili si sahihi naomba tusaidiane katika hili ili tusiwagawe wala kuwachanganya watanzania”
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari –Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo ametoa wito kwa waandishi wa habari kuepuka kuingilia majukumu ya taasisi nyingine kwa kugeuka kuwa mahakama.
“Baadhi ya magazeti hapa nchini wakati mwingine yanageuka kuwa mahakama kwa kuwahukumu watu, huu sio uandishi bora wa habari” Amesisitiza Bw. Hokororo.
Amewataka waandishi wa habari na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini kuzingatia weledi wa taaluma ya habari kwa kuwaachia wanananchi wenyewe kuamua juu ya masuala muhimu yenye mustakabali wa taifa lao badala ya kuwaamulia.
Ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha kuwa wanawajengea uwezo waandishi wa habari walio katika vyombo vyao kwa kuwaendeleza kielimu na kuwapatia vifaa vya kisasa ili viweze kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa magazeti hayo Bw. Kiondo Mshana ameushukuru uongozi wa Idara ya Habari kwa kuwa na program ya kuvitembelea vyombo vya habari hapa nchini huku akibainisha kuwa ni fursa ya pekee inayojenga mahusiano mema baina ya serikali na vyombo vya habari.
“Ninashukuru sana kwa ujio wenu na kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya hapa nchini, kwa upande wetu mmetueleza mambo makubwa, kwetu hii ni shule tosha na tumejifunza mengi kutoka kwenu naomba tuendelee kuwasiliana ili tuifikisha nchi hii mahali pazuri”
Ametoa wito kwa wahariri na waandishi wa habari kote nchini kuzingatia weledi wa taaluma ya habari kwa kuepuka kuandika habari za hisia na chuki ili kuepusha madhara katika jamii na kusisitiza kuwa atahakikisha vyombo anavyovisimamia vinatanguliza masllahi ya taifa.
“Gazeti la Guardian ni kioo cha jamii , linasomwa na watu wengi ndani na nje ya nchi, mimi kama mkurugenzi mkuu siwezi kuruhusu habari zinazolenga kuwagawa wananchi zisizo na maslahi kwa taifa zichapishwe, taifa hili ni letu sote machafuko yakitokea nchini hayabagui mwandishi wa habali na asiye mwandishi sote tunapata msukosuko ” Amesisitiza Bw. Mshana.
Kuhusu suala la elimu na maadili kwa wafanyakazi walio chini yake ameeleza kuwa yeye kama kiongozi anaendelea kulipa kipaumbele kwa kutoa msisitizo kwa watumishi wote wa vyombo hivyo kuzingatia maadili ili jamii iendelee kuiheshimu taaluma ya habari.
Naye muhariri Mtendaji wa gazeti hilo Bw. Wallace Mauggo ameiomba serikali kuendelea kuijengea uwezo Idara ya Habari ili iweze kutekeleza majukumu yake bila vikwazo vyovyote kutokana na umuhimu mkubwa ilio nao kwa taifa na tasnia ya habari.
MWISHO.