Watoto wa Mitaani Tanzania Wang’ara Brazil, Taifa Stars V Burundi Aprili 26

Watoto wa Mitaani Tanzania Wang'ara Brazil

Watoto wa Mitaani Tanzania Wang’ara Brazil

TIMU ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.
 
Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.
 
Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Aprili 6 mwaka huu.
Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa Aprili 5 mwaka huu ni Burundi itakayocheza na Pakistan.
 
Katika mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines mabao 2-0.

TAIFA STARS, BURUNDI KUCHEZA APRILI 26
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.
 
Baadaye wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho kitakachoivaa Burundi.
 
Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka nchini Kenya.