Na Veronica Kazimoto, Morogoro
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ametoa wito kwa Wamiliki wa viwanda nchini kutoa ushirikiano kwa Wadadisi na Wasimamizi wa Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Viwanda inayotarajia kufanyika mwezi Septemba, 2014.
Akiwahutubia Wasimamizi na Wadadisi wakati wa kufunga mafunzo ya zoezi hilo mkoani Morogoro, Bendera amesema ni muhimu kwa Wamiliki wa viwanda kutoa ushirikiano kwa wadadisi ili kuhakikisha kuwa Serikali inapata takwimu sahihi ya orodha ya viwanda vilivyopo nchini.
“Natoa wito kwa Wamiliki wote wa viwanda nchini kutoa ushirikiano kwa Wadadisi kwa kuwapatia takwimu sahihi za viwanda vyao, wakifanya hivyo, zoezi hili litafanikiwa kwa ufanisi mkubwa sana” amesema Bendera.
Aidha, Bendera amewatoa wasiwasi Wamiliki wa viwanda kwa kusema kuwa zoezi hili la Uorodheshaji wa Viwanda halitaathiri shughuli zozote za viwandani.
Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morice Oyuke amesema, baadhi ya taarifa zitakazokusanywa katika zoezi hilo ni pamoja na anuani za viwanda, mahali viwanda vilipo, aina ya umiliki na utaifa wa mmiliki.
Taarifa nyingine ni gharama za malipo mbalimbali kwa wafanyakazi, mapato yanayotokana na uzalishaji, mwaka kiwanda kilipoanzishwa, aina ya bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi na gharama za uzalishaji. Zoezi la Uorodheshaji wa Viwanda linahusu viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na litafanyika nchi nzima kwa muda wa miezi miwili kuanzia mwezi huu Aprili mpaka Juni, 2014.