Liverpool inaweza kuwa bingwa, usibishe sana!

liver

BAADA ya kuichapa Tottenham mabao 4-0 juzi usiku kwenye Uwanja wa Anfield, maneno yametanda duniani kote kwamba huenda huu ni msimu wa Liverpool.

Yoyote atakayesema hivyo anaweza asiwe mbali sana na ukweli kwa sababu kuna dalili zote.

Daglish aliwahi kufanya hivi

Wamewahi kufanya hivi kabla. Katika msimu wa 1985-86 kikosi cha kocha Kenny Dalglish kilikuwa kimeachwa nyuma kwa idadi ya pointi tano na wapinzani wao wa jadi Everton huku zikiwa zimebaki mechi 13.

Pengo hilo liliongezeka kufikia pointi nane baada ya kuchapwa 2-0 na Everton katika uwanja wao wa nyumbani Anfield. Lakini kuanzia hapo walishinda mechi 11 na kutoa sare moja huku wakitwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi mbili kileleni dhidi ya Everton iliyokuwa inafundishwa na kocha Howard Kendall.

Ni kama ilivyo sasa ambapo Liverpool imeshinda mechi nane mfululizo.

Nyumbani hatoki mtu

Liverpool ndio timu ya pili kwa kuwa na rekodi nzuri katika uwanja wake wa nyumbani. Na hapo hapo bado Manchester City na Chelsea inabidi zifunge safari kwenda Anfield.

Na kama ambavyo Jose Mourinho anavyoendelea kusema kwamba timu yake haiwezi kushinda taji msimu huu. Kama Liverpool akiwapiga wote wawili basi ubingwa utakuwa mikononi mwake mwenyewe na si kwa kumtegemea mtu mwingine.

Ukitaka kujua kuwa Chelsea na Manchester City huenda wanasubiri vichapo basi angalia jinsi ambavyo Liverpool amezipiga timu nzito kama Manchester United, Arsenal na watani wao wa jadi Everton.

source: mwanaspoti