WAZEE: Moyes adai kikosi cha Man United kimejaa wazee

moyes

KOCHA, David Moyes amesema hata Sir Alex Ferguson asingefanya kitu kwenye kikosi cha sasa cha Manchester United kutokana na wachezaji wengi wazee.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England wamefanya vibaya msimu huu na hadi sasa wakiwa wamelamba vichapo 10.

Mashabiki wa timu hiyo walionekana kuchukia na kupitisha ndege iliyokuwa na bango linalomtaka Moyes aondoke Old Trafford. Hata hivyo, Moyes alisema hata Ferguson angeendelea na kazi uwanjani hapo asingefua dafu kwa kikosi hicho kilichopo Old Trafford kwa sasa.

“Hata Sir Alex angekuwa hapa ungekuwa mwaka mgumu kwake, analifahamu hilo,” alisema Moyes.

“Kila mtu anafahamu kikosi kina wachezaji wengi wazee, hivyo ni wazi ungekuwa msimu mgumu kwa kocha yeyote yule ambaye angekuwa hapa.”

Moyes alifahamu mapema mpango wa mashabiki kupanga kupitisha ndege uwanjani Old Trafford kabla ya mechi yao dhidi ya Aston Villa juzi Jumamosi na kusema kwamba wapo huru kubainisha hisia na mawazo yao.

“Mashabiki wengi wa Manchester United wanakerwa na hali ilivyo, hivyo siku zote anachohitaji sisi tucheze vizuri na wanataka matokeo mazuri,” alisema na kuongeza. “Kitu kizuri ni kwamba watu watakaoamua ni wale walionichagua.

“Watu hao ni wenye akili sana. Kwa kifupi mtu mwenye akili zaidi ni yule aliyenipa kibarua hiki (Ferguson).”

source:mwanaspoti