UINGEREZA inajivunia kuwa nchi inayoongoza katika uwekezaji nchini Tanzania na itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kiuchumi na kuleta maendeleo. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amemuambia Rais Kikwete wakati wa mazungumzo yaliyofanyika 10 Downing Street, Machi 31, 2014, ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya Waziri Mkuu wa Uingereza.
“Tunafurahia sana uhusiano wetu na kujivunia kuwa tunaongoza katika Uwekezaji nchini Tanzania” Bw. Cameron amesema na kumhakikishia Rais Kikwete kuwa Uingereza iko tayari kutoa misaada zaidi.
Rais Kikwete amewasili nchini Uingereza tarehe 30 Machi, 2014 kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku 3 kufuatia mualiko wa Bw. Cameroon ambaye pia amemuomba Rais Kikwete aendelee kutoa mchango wake wa mawazo katika masuala ya kimataifa hasa baada ya mwisho wa muda wa malengo ya millennium ya 2015.
“Tunakaribia mwisho wa muda wa malengo ya millennia Mwaka 2015, tutahitaji kuweka vipaumbele vingine baada ya hivyo kama kuondosha umaskini, Maji safi na salama, masuala ya ufisadi na utawala bora, natumaini utaendelea kutoa mchango wako baada ya malengo hayo kufikia tamati” Waziri Mkuu Cameron amemuambia Rais Kikwete ambapo Rais amekubali ombi hilo na kuahidi ushirikiano wake.
Mapema leo asubuhi Rais amekutana na mtoto wa Mfalme Prince Andrew katika makazi ya Malkia ya Buckingham ambapo wamebadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali ya Kimataifa na Kijamii.
Kabla ya kwenda Buckingham Rais amefungua mkutano kuhusu uwekezaji na kuelezea fursa na nafasi zilizopo za uwekezaji nchini Tanzania na kuelezea kwanini wawekezaji watakuwa wanafanya uamuzi bora kwa kuwekeza Tanzania kuwa ni pamoja na;
“Fursa nyingi, amani, usalama, soko la kutosha na kubwa kwa vile Tanzania iko katika Umoja wa Afrika Mashariki, Ukanda wa Maziwa Makuu na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika,hivyo kuwa na uhakika wa soko kubwa na pana” amesema.
Katika ziara yake Rais pia amekutana na Mstahiki Meya wa Jiji la London Mama Alderman Fiona Woolf na kukaribishwa rasmi Jijini London. Mstahiki Meya anatarajia kutembelea Tanzania, Mwezi Septemba Mwaka huu.
Rais alipowasili London tarehe 30 Machi,2014, alikutana na Watanzania wanaoishi nchini Uingereza na kuwaeleza maendeleo yaliyopo nchini Tanzania. Rais anaendelea na ziara yake nchini Uingereza.