Yohane Gervas, Rombo
WAKAZI wa Kijiji cha Ngoyoni Kata ya Ngoyoni Tarafa ya Mengwe, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wameipongeza Serikali wilayani humo kwa kuwaondolea kero ya maji iliyodumu kwa muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili.
Neema hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo kufungua rasmi kisima kikubwa cha maji katika Kijiji cha Ngoyoni Kata ya Ngoyoni Tarafa ya Mengwe. Diwani wa kata hiyo, Protas lyakurwa akitoa shukrani hizo kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho mbele ya mkuu wa wilaya, Elinas Pallengyo alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia huduma hiyo muhimu ya maji kwani kabla ya kuwepo kwa kisima hicho wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Aidha Lyakurwa alisema kuwa wanafunzi walikuwa wakilazimika kuacha vipindi vya darasani kwa ajili ya kwenda kutafuta maji jambo ambalo lilikuwwa likishusha kiwango cha elimu katika kijiji cha ngoyoni.
Awali Mhandisi wa maji wa wilaya ya Rombo, Andrew Tesha akisoma taarifa ya mradi wa kisima hicho amesema kuwa ujenzi wa kisima hicho ambao umegharimu zaid ya shilingi milioni sabini na mbili, utawanufaisha wakazi elfu moja wa kijiji cha Ngoyoni ambao ni sawa na asilimia 43
Wakati huo huo; Wananchi wanne wakazi wa Kijiji cha Mengwe chini wakiongozwa na Mhandisi wa Maji wilayani Rombo, Andrew Tesha wamejitolea kupanda miti takribani mia tatu kuzunguka katika chanzo cha maji cha kiunikoni kilichopo katika Tarafa ya Mengwe wilayani Rombo.
Akitoa Taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo, mhandisi wa maji wa Wilaya ya Rombo, Andrew Tesha amesema kuwa miti hiyo ambayo ni Rafiki ya maji ilipandwa mwishoni mwa wiki iliyopita kuzunguka eneo la chanzo cha maji cha kifunikoni wakiwa na lengo la kulinda chanzo hicho
kisikauke.
Aidha Tesha amesema kuwa wakati wa zoezi hilo walipata changamoto kadhaa ikiwemo ya mwamko mdogo au ushirikiano hafifu kati ya wananchi kwani katika zoezi hilo ni wananchi wanne tu ndio waliojitokeza kushirikiana nae kupanda miti hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinas Pallengyo alisema ili huduma ya maji iwe endelevu wananchi hawana budi kutunza vyanzo vya maji vilivyopo kwa kupanda miti. Aidha ameongeza kuwa sula la utunzaji wa mazingira si la serikali peke yake bali kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki tena kwa hiyari yake.