Liverpool yaishusha Chelsea

fulham

Kiungo wa Fulham, Ashkan Dejagah (kulia) akimpita beki wa Everton, John Stones wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Craven Cottage jana Jumapili. Everton ilishinda 3-1. Picha na AFP

LIVERPOOL imeiporomosha Chelsea kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya jana Jumapili kuichapa Tottenham Hotspur mabao 4-0 uwanjani Anfield na kuweka pengo la pointi mbili juu.

Mabao ya Younes Kaboul, aliyejifunga katika dakika ya pili ya mchezo kabla ya Luis Suarez kufunga bao lake la 29 msimu huu kwenye dakika 25 yalitosha kwa Liverpool kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kaboul alijifunga kwa kisigino alipojaribu kuokoa krosi ya chini chini iliyopigwa na Glen Johnson kutoka upande wa kulia, kabla ya Suarez kutumia makosa ya beki Michael Dawson, aliyekuwa ameingia sekunde chache tu kuchukua nafasi ya Vertonghen aliyeshindwa kuendelea na mchezo kutokana na kuumia. Kipindi hicho cha kwanza kiliendelea kushuhudia kosa kosa nyingi, ikiwamo mpira wa kichwa wa Suarez kuokolewa na kipa Hugo Lloris na kugonga mwamba kabla ya beki kuokoa.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 10 tu baada ya mapumziko, kiungo Mbrazili Philippe Coutinho alifunga bao maridadi kwa shuti kali baada ya kuingia na mpira ndani ya 18 ya goli la Spurs. Liverpool iliendelea kulisakama goli la Spurs na kiungo Jordan Henderson alifunga bao la nne katika dakika 75 kwa mpira wa faulo.

Ushindi huo umeifanya Liverpool msimu huu kuzoa pointi zote sita kutoka kwa Spurs baada ya mchezo wa kwanza kushinda mabao 5-0 uwanjani White Hart-Lane. Liverpool kwa sasa imeketi kwenye kilele cha ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 71 kwenye mechi 32.

Kipigo cha bao 1-0 cha Chelsea dhidi ya Crystal Palace kimekuwa pigo kubwa kwao na kuporomoshwa kileleni, sawa na sare ya bao 1-1 iliyopata Manchester City kwa Arsenal imewatibulia nafasi ya kuwashusha zaidi Chelsea na wao kushika namba mbili. Hata hivyo, Man City ina michezo miwili mkononi.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo uliofanyika jana Jumapili, Everton imeendeleza matumaini yao ya kuingia kwenye nne bora baada ya kuichapa Fulham mabao 3-1 uwanjani Craven Cottage.

Bao la kujifunga la David Stockdale na mawili ya wakali Kevin Mirallas na Steven Naismith yalitosha kwa Everton kushinda na kujiimarisha kwenye nafasi ya tano, pointi nne pungufu kuifikia Arsenal kwenye nafasi ya nne, lakini wababe hao wa Goodison Park wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Fulham ilishinda bao lake kupitia kwa Ashkan Dejagah.
Source: http://www.mwanaspoti.co.tz/