Baadhi ya waandamanaji wakiimba na kucheza kabla ya kuzuka kwa vurugu na FFU kulazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.
Mwandishi Wetu, Arusha
MADEREVA wa daladala (maarufu kama vifodi) mkoani Arusha jana walifanya mgomo wakupinga kitendo cha kutozwa fedha kiasi cha Sh 5,000 hadi 10,000 na Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani hata kama magari yao hayana makosa.
Walidai endapo baadhi ya madereva wanashindwa kutoa kiasi hicho cha fedha (notefication) wamekuwa wakipelekwa jela miezi mitatu mpaka sita. Mgomo huo ulianza jana asubuhi saa 11:00 alfajiri mjini hapa, huku madereva wakihoji kwanini wanafanyiwa hivyo ilhali hakuna vituo vya kushusha na kupakia abiria.
Walisema licha ya wao kukamatwa, lakini uongozi wa manispaa imeendelea kukusanya ushuru bila kuufanyia kazi ikiwemo ujenzi wa stendi za vifodi, ambayo ingeweza kuwa suluhisho la mvutano huo.
Adha kubwa ilikuwa kwa baadhi ya wakazi ambao hutumia usafiri huo, kwani walilazimika kutembea kwa miguu na wengine kutumia usafiri wa pikipiki (maarufu kama bodaboda) baada ya daladala kugoma kufanya safari zake katika maeneo mbalimbali.
Baadaye polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi baada ya madereva kuanza kutishia amani majira ya saa saba mchana ambapo walianza kuyatupia mawe baadhi ya magari yaliyokuwa yakitoa msaada wa kubeba abiri.
Ndipo FFU walilazimika kutumia virugu na mabomu ya machozi kuwadhibiti, hali iliyozua tafrani kubwa na kuwa kero kwa wapitanjia wengine.