Na Magreth Kinabo –MAELEZO, Dodoma.
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Anne Makinda ametoa changamoto kwa wajumbe wenzake wanawake walio kwenye Bunge hilo, kujenga hoja zenye nguvu zinazohusu masuala yanayohusu wanawake na kuzitetea kwa sauti moja ili ziweze kupita katika Rasimu ya Katiba.
Kauli hiyo imetolewa na Anne ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akitoa mchango wake kwa wajumbe wa semina ya kujenga agenda muhimu kwa masuala ya kijinsia iliyoandaliwa na Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (TWPG) kwa wajumbe wanawake wa Bunge hilo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa.
“ Ninawaomba tuwe na hoja zenye nguvu wakati wakuchangia mjdala wa Rasimu ya Katiba . Tukisimama kwa hoja za nguvu na kutetea vifungu vinavyohusu masuala ya wanawake tunaweza kubadilisha vifungu. Tuzungumzeni hoja tuache kufanya fujo, tusiingie katika malumbano ambayo hayana tija, tuache kuzomea tukifanya hiyo tutakuwa tumejijengea heshima,” alisema Mama Anne.
Kwa upande wake mmoja wa mtoa mada katika semina hiyo,kuhusu haki za wanawake, utu, hali ya maisha na mgawanyo wa rasilimali, Ussu Mallya, ambaye pia ni wanaharakati wa masuala ya wanawake aliwataka wajumbe hao ,wanawake kutetea saula la Usawa wa Kijinsia liingizwe katika Rasimu ya Katiba likiwa ni moja ya Tunu za Taifa.
Mtoa mada mwingine ambaye pia mjumbe Bunge hilo na ni Makamu Mwenyekiti wa TWPG, Suzan Lyimo alisema ni vema wanawake hao kupigania asiliamia 50 inakuwepo ili kuhakikisha masuala yote yanayohusu wakina mama yakuwemo, mfano kwenye nafasi za ubunge, ajira na ngazi zingine za maamuzi.
Suzan alisema hayo wakati akitoa mada kuhusu Uwakilishi wa wanawake, katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mada nyingine iliyotolewa katika semina hiyo ni masuala ya miradhi na ndoa iliyotolewa na Victoria Mandari kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania(TAWLA) ambaye aliwataka wajumbe hao kutoendeleza mambo ya mila na desturi ambayo yanamkandamiza mwanamke.
Katika semina hiyo, baadhi ya wanawake hao walipendekeza masuala ya haki ya elimu kwa wanawake, haki za uzazi salama, haki ya kumiliki mali, haki ya ulinzi kwa wanawake na watoto, haki ya mtoto wa nje ya ndoa, umri wa mtoto kuolewa kuwa ni miaka 18 kuingia katika rasimu hiyo.