Mama Tunu  Pinda awaasa wanandoa

“Ndoa zisipokuwa imara watoto wanakosa malezi, ndoa zinapovunjika, si wanadoa tu wanaoharibikiwa, bali watoto

“Ndoa zisipokuwa imara watoto wanakosa malezi, ndoa zinapovunjika, si wanadoa tu wanaoharibikiwa, bali watoto

MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewaeleza wanandoa kuwa ndoa ndiyo taasisi ya kwanza kuwafundisha watu maadili na kumjua Mungu pasipo Mungu haiwezekani.

Amesema hayo wakati akifungua rasmi semina ya wanandoa wa kuanzia siku moja hadi miaka 25 iliyoandaliwa na watoa huduma wa New Life in Christ (Maisha Mapya Ndani ya Kristo) jana mchana tarehe 29 Machi, 2014 katika Ukumbi wa Msimbazi Centre jijini Dar es salaam.

“Ndoa ndiyo Taasisi ya msingi na ya kwanza kabisa kati ya Taasisi zote katika jamii ya mwanadamu ambayo ilianzishwa na mwenyezi Mungu”, alisema Mama Pinda.

Taasisi hii ni muhimu sana kwani ndiyo chanzo cha Familia na ndio chanzo cha jamii ya watu na mataifa mbalimbali hivyo wanandoa wote inawapasa kuwa wa kwanza katika kukuza maadili kwa kufuata maandiko ya mwenyezi mungu.

Mama Tunu Pinda alisema, katika Kitabu cha Mwanzo, sura ya kwanza aya ya 27-28 inasema kwamba mungu aliwaumba mtu mume na mtu mke kisha akawabariki akisema: “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze Dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi”
“Wanandoa  hamnabudi kujenga maadili mazuri,masikilizano na uvumilivu katika ndoa ili muweze kuepusha uvunjifu wa maadili katika ndoa”. Inaaminiwa kwamba matatizo mengi ya kuporomoka kwa maadili katika ndoa chanzo chake kikubwa ni kukosekana kwa uvumilivu, alifafanua Mama Pinda.

“Ndoa zisipokuwa imara watoto wanakosa malezi, ndoa zinapovunjika, si wanadoa tu wanaoharibikiwa, bali watoto pia hupata majeraha makubwa ya kisaikolojia katika maisha yao,hivyo nawaomba wanandoa kuisha katika imani na masikilizano ili kuweza kudumisha ndoa zenu”, alisisitiza.

Semina hii ni chachu na sehemu muhimu sana ya kujifunza na kukumbushana masuala muhimu ya kujenga ndoa zenu, hivyo mtumie nafasi hii kutafakari hali halisi ya ndoa zenu kwa kuwa wasikivu na wachangiaji wa mawazo na pia kwenda kuwaeleza na wengine kile mlichojifunza: “Naamini semina hii italeta uponyaji na nuru mpya katika ndoa zenu na familia na kuwa kichocheo katika kuimarisha ndoa zenu”, alisema.

Napenda kusisitiza kwamba, hatuwezi kuwa na Taifa la watu wenye maadili mema kama ndoa zenu ambazo ni kiini cha familia, jamii na Taifa hazitaimarishwa, ni dhahiri kwamba hatutaweza kupata viongozi bora ikiwa ndoa zilizo imara ambazo ni kiini cha uhai wa familia zitaachwa ziyumbe:” Viongozi bora hutoka kwenye ndoa bora ni vizuri kujenga utamaduni katika jamii kwa kuwa na ndoa zisizotetereka”alisema Mama Tunu.

Mama Pinda aliwaomba watoa huduma wa “New Life in Christ” pamoja na makanisa na watu wengine wanaotoa huduma za mafundisho ya uimarishaji wa ndoa kufanye jambo hili kuwa endelevu na kuhusisha ndoa nyingi kadri iwezekanavyo. “Serikalini  wanasema Matokeo ya Haraka sasa au Big Results Now nami nashauri iwe hivo katika ndoa zenu yawe malengo yenu na yaelekezwe katika kuleta Matokeo Makubwa Zaidi”, aliongezea Mama Tunu Pinda.

Mama Pinda aliwashauri watoa huduma wa “New Life in Christ”, kuangalia namna ya kuandaa Semina kwa ajili ya vijana ambao sasa wameingia katika ulimwengu wa utandawazi kwa kuwaaandaa na kuwasaidia waingie kwenye taasisi ya ndoa kwa kumshirikisha Mungu kupata wenza wao kuliko kutafuta wachumba kupitia mitandao ya kijamii kama vile facebook, viber, Instagram na mingineyo. “Semina hizi zitawasaidia kuwajenga kimaadili huku wakitambua majukumu yao kama mume  ama mke, kama baba au mama na hatimaye kuishi katika maadili mema”.

Mapema, Mwenyekiti wa “New Life in Christ” Dkt. Alyson Mmanyi alisema huduma kama hizi za semina zinatolewa kwa watu wote wakristo wa madhehebu mbalimbali ili kuweza kunusuru ndoa na uvunjifu wa maadili kwani Taasisi ya ndoa imevamiwa na ndoa bila Mungu haiwezekani.

”Tumekuwa tunatoa huduma za kuhubiri Injili kwa watu mbalimbali ambapo tayari tumeshatoa huduma hizi Mkoani Tarime, Rorya na tunatarajia kwenda Butiama mwaka huu”,alisema Dkt. Alyson.
 
……………………………