NCHI WANACHAMA WA UMOJA WA ULAYA (EU) zimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuanzisha na kusimamia vizuri Mchakato wa Kutungwa Katiba Mpya Tanzania ambao unaendelea nchini.
Pongeza za nchi hizo zimetolewa leo Ijumaa, Machi 28, 2014, Ikulu, Dar Es Salaam wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Rais Kikwete na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao za Ulaya katika Tanzania katika mkutano unaojulikana kama Majadiliano ya Kisiasa kati ya Tanzania na EC (EU-Tanzania Political Dialogue).
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mwanzoni mwa mkutano huo uliochukua kiasi cha saa mbili, Mwakilishi wa EU katika Tanzania, Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi amemwambia Rais Kikwete.
“Hata kwa sisi ambao siyo wadau wa moja kwa moja katika mchakato huu, tunaona, tunajua na tunaamini kuwa umefanya kazi yenye kustahili pongezi sana – ya kuanzisha na kuendelea kusimamia Mchakato wa Katiba Mpya. Tunakupogeza sana Mheshimiwa Rais.”
Katika Mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Mabalozi hao wamefanya mazungumzo chini ya mkutano wa kila mwaka unaojulikana rasmi kama “EU-Tanzania Political Dialogue ambao ulianzishwa rasmi na kipengele cha nane cha Mkataba wa EU na Afrika.
Mkutano huo umejadili mambo matano muhimu ambako kila upande umeelezea uelewa na msimamo wake kuhusu mambo hayo matano ambayo ni Mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea nchini, Hali ya Haki za Binadamu,Mazingira ya kufanyia Biashara katika Tanzania na Rushwa, Masuala ya Kikanda na Hali ya Ukraine.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amewaelezea mabalozi hao juu ya maendeleo ya mchakato wa Katiba akisisitiza kuwa mpaka sasa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaendelea kutafuta kufikia makubaliano ya kanuni na taratibu. “Sote tunasubiri kuona wanaanza kazi rasmi ya kutunga Katiba, shughuli ambayo haijaanza.”
Rais Kikwete pia amechukua nafasi hiyo kuwaelezea Mabalozi hao kuhusu maeneno ya msingi ambayo yanatakiwa kuangaliwa na Serikali Mbili ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo ya manung’uniko ya pande zote mbili.
Mabalozi hao pia wameeleza msimamo na kutaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu kile kinachoonekana kama misuguano ya kidini, imani ndogo ya Wananchi katika taasisi za Polisi na Mahakama, na msimamo wa Serikali kuhusu sheria mpya ya habari.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais Eduardo Dos Santos wa Angola. Ujumbe huo umewasilishwa kwa Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mheshimiwa Manuel Agusto.